Mwambata wa kijeshi wa Uturuki huko Israel alipanga jaribio la mapinduzi
Duru za habari za Kizayuni zimetangaza kuwa mmoja wa waliopaga jaribio la mapinduzi ya serikali huko Uturuki alikuwa ni mwambata wa kijeshi wa nchi hiyo huko Israel.
Gazeti la Kizayuni la Times Israel limeripoti kuwa Akin Ozturk Kamanda wa zamani wa kikosi cha anga cha Uturuki ambaye ni mmoja wa wapangaji wakuu wa jaribio la mapinduzi lililoshindwa huko Uturuki, alikuwa mwambata wa kijeshi wa Uturuki huko Israel baada kustaafu jeshini mwaka jana.
Akin Ozturk kamanda wa zamani wa jeshi la anga la Uturuki alitiwa mbaroni jana kwa tuhuma za kuhusika katika jaribio la mapinduzi lililoshindwa huko Uturuki.
Ozturk alifanya kazi ya mwambata wa kijeshi wa Uturuki katika ubalozi wa nchi yake huko Tel Aviv kati ya mwaka 1998 hadi 2000 na baada ya hapo, yaani kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 mwanajeshi huyo aliteuliwa kuwa kamanda wa Jeshi la Anga la Uturuki . Akin Ozturk mwenye umri wa miaka 64 mwaka jana alijiuzulu nafasi ya kamanda wa jeshi la anga la Uturuki na akawa anafanya kazi katika Baraza Kuu la Kijeshi la Uturuki.
Juzi usiku wanajeshi kadhaa wa Uturuki walifanya jaribio la kuipindua serikali ya Rais Recep Tayyep Erdogan wa nchi hiyo, kisha baadhi ya askari jeshi walimiminika mitaani katika miji ya Istanbul na Ankara na kutangaza kuwa wao ndio wanaoiongoza nchi. Hata hivyo wananchi wa Uturuki waliingia mitaani na hivyo kuzima jaribio hilo la mapinduzi.