Hali ya kutisha ya zama za mwisho huko Gaza
Huku nchi za Magharibi zikiunga mkono jinai zinazoongezeka kila siku za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina hasa katika kuwalazimisha watu wa Gaza kuyahama makazi yao, weledi wa mambo wanasema wigo wa jinai hizo unaweza kuzikumba nchi hizo pia baada ya muda usio mrefu.
Baada ya kupita siku 311 tangu utawala ghasibu wa Israel unaokalia Quds Tukufu kwa mabavu kuanzisha vita vya maangamizi ya kimbari dhidi ya Gaza, ofisi ya vyombo vya habari ya serikali ya Palestina katika Ukanda wa Gaza imewasilisha takwimu za kutisha za jinai za kivita za utawala huo ghasibu na mauaji ya raia wa Palestina.
Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa, zaidi ya jinai 3,486 zimefanywa na Wazayuni katika kipindi cha miezi 10 iliyopita huko Gaza ambapo kutokana na jinai hizo, zaidi ya Wapalestina 49,897 wameuawa shahidi au kutoweka, ambapo hatima ya takriban watu elfu 10 haijulikani huku miili ya mashahidi zaidi ya 39,897 ikiwa imetambuliwa katika hospitali mbali mbali za ukanda huo.
Wanawake na watoto ni asilimia 69 ya wahanga wa mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza. Taarifa hiyo inasema watoto 16,456 ni miongoni mwa waliouawa shahidi huku wanawake waliouawa shahidi wakiwa ni 11,088. Hivi sasa zaidi ya watoto 17,000 wa Kipalestina wamepoteza mzazi mmoja au wote wawili kutokana na mashambulizi ya Wazayuni. Hali kadhalika watoto 3,500 wa Kipalestina pia wako katika hatari ya kuuawa kutokana na utapiamlo na ukosefu wa chakula. Pia zaidi ya wanawake 60,000 wa Kipalestina wanaoishi Gaza ni wajawazito na wako hatarini kutokana na ukosefu wa huduma muhimu za afya.
Aidha miongoni mwa waliouawa shahidi katika hujuma ya kinyama ya Israel dhidi ya Gaza wapo wafanyakazi wa sekta ya afya wapatao 885 na pia wamo wafanyakazi 79 wa huduma za kiraia. Vilevile, utawala haramu wa Israel ili kuzuia taarifa za jinai zake kuwafikia walimwengu, umeua waandishi habari 168 huko Gaza.
Hadi sasa, takriban makaburi saba ya halaiki yametambuliwa ndani ya hospitali za Gaza, na miili ya mashahidi 520 imefukuliwa kutoka kwenye makaburi hayo ya halaiki.
Pia mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika kipindi cha siku 311 zilizopita yamewajeruhi Wapalestina 92,152. Majeruhi 12,000 ndani ya Ukanda wa Gaza wanahitaji matibabu ya dharura nje ya ukanda huo. Zaidi ya wagonjwa 10,000 wa saratani wanakabiliwa na hatari ya kifo kutokana na ukosefu wa dawa muhimu. Mbali na idadi hii, zaidi ya wagonjwa 3,000 wanahitaji kutumwa nje ya Gaza kwa matibabu ya haraka.
Mbali na mashambulizi yake ya kinyama, utawala wa Kizayuni unazuia kuingizwa dozi milioni moja na elfu 300 za chanjo huko Gaza. Zaidi ya wagonjwa 350,000 wa muda mrefu pia wanakabiliwa na hatari ya kifo kutokana na ukosefu wa dawa za kutosha.
Tokea uanzishe vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza Oktoba saba mwaka jana, utawala wa Kizayuni umewatia mbaroni zaidi ya wakazi 5,000 wa Ukanda wa Gaza, 310 kati yao wakiwa ni wafanyakazi wa afya na 36 kati yao ni waandishi wa habari.
Katika muda wa siku 311 zilizopita, zaidi ya wakazi milioni 2 wameyakimbia makazi yao katika Ukanda wa Gaza. Wavamizi hao wa Kizayuni wameharibu kabisa vituo 198 vya serikali na kuharibu kikamilifu shule na vyuo vikuu 121. Aidha wameharibu vibaya shule na vyuo vikuu 333 kwa mashambulizi yao ya roketi na mizinga.
Utawala dhalimu wa Israel pia umesambaratisha kikamilifu zaidi ya nyumba 150,000 katika mashambulizi yake ya makombora na mizinga. Mbali na idadi hii, nyumba 80,000 zimeharibiwa kwa njia ambayo haziwezi tena kukalika bila kukarabatiwa. Pia, nyumba zingine 200,000 zimeharibiwa kiasi.
Katika muda wa siku 311 za mashambulizi yao ya kinyama, Wazayuni katili wamedondosha tani 82,000 za mabomu dhidi ya watu wa Gaza. Kufuatia mashambulizi hayo ya kinyama hospitali 34 za Gaza hazitumiki tena. Mbali na hayo, vituo vya afya 80 na taasisi za matibabu na afya 162 zimelengwa na wavamizi hao na hivyo haziwezi tena kutoa huduma.
Wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni wa Israel pia wameharibu turathi za kale zipatazo 206 katika Ukanda wa Gaza. Mbali na hayo wavamizi hao Wazayuni wameharibu kilomita 330 za njia ya usambazaji umeme huko Gaza. Katika kuendeleza jinai zao, Wazayuni wamebomoa vituo 34 vya michezo na hawakukomea hapo bali pia wameharibu visima zaidi ya 700 vya maji kote Gaza.
Takwimu hizo za kuogofya zinaonyesha wazi kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unatekeleza jinai zake kwa lengo la makusudi la kuifanya Gaza iwe eneo lisiloweza kukalika kwa wanadamu na hivyo kuwalazimisha Wapalestina kuondoka katika ardhi yao hiyo ya jadi na kuhamia Misri au nchi nyinginezo. Utawala wa Kizayuni ulikuwa umeficha nia yake hiyo miezi michache iliyopita, na sasa, ingawa hautangazi wazi wazi, lakini kwa hakika unachukua hatua katika mwelekeo huu wa maangamizi ya kimbari. Matamshi ya hivi karibuni ya Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa pia ni uthibitisho wa ukweli huo.
Farhan Haq huku akigusia sura pana ya maagizo ambayo limepokea jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuwafurusha wakazi wa Ukanda wa Gaza, amesema kuwa amri hizo zinajumuisha eneo la takriban kilomita za mraba 305 au karibu asilimia 84 ya Ukanda wa Gaza.
Pamoja na hayo yote, ifahamike kuwa hatari zinazosababishwa na kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni hazitaishia tu kwa watu wa Gaza na kuhamishwa kwao kwa nguvu, bali pia zitazifikia nchi za Ulaya, jambo ambalo linafanya kimya cha nchi hizo na kuridhika kwao na jinai hizo za Wazayuni kutokuwa sahihi hata kidogo.