Wananchi wa Yemen wafanya maandamano makubwa kuilaani Marekani
Maelfu ya wananchi wa Yemen wamefanya maandamano mjini San'a kulaani kuendelea mashambulizi ya kivamizi ya Saudi Arabia na Marekani nchini mwao.
Waandamanaji wamepiga nara za kuilaani Marekani wakisema inakwamisha mazungumzo ya amani. Pia wamepiga nara wakisema: "Kamwe hatutaipigia magoti Marekani."
Licha ya ukatili mkubwa wanaofanyiwa na madola vamizi, lakini bado wananchi wa Yemen wako imara na hawasiti kujitokeza kwa wingi kuonesha hisia zao kila inapobidi kufanya hivyo.
Wakati huo huo harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah imesema kuwa, mazungumzo ya kusaka amani ya nchi hiyo hayawezi kufanikiwa kama harakati hiyo haitafanya mazungumzo ya moja kwa moja na Saudi Arabia kwani ndiye mkwamishaji wa mazungumzo ya amani yanayoendelea nchini Kuwait.
Wiki iliyopita, harakati ya Ansarullah ilianza mazungumzo na kundi linaloungwa mkono na Saudi Arabia la Abdu Rabbuh Mansru Hadi nchini Kuwait, baada ya mazungumzo hayo kukwama kwa muda wa wiki mbili.
Hata hivyo, mkuu wa timu ya harakati ya Ansarullah katika mazungumzo hayo, Muhammed Abdulsalam alisema jana kuwa, mazungumzo hayo ya Kuwait ni ya kupoteza muda, kwani muhusika mkuu wa uvamizi wa Yemen, yaani Saudi Arabia, hashiriki moja kwa moja.
Amesema, timu yake iko tayari kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Saudia ambayo ndiye muhusika mkuu wa uvamizi na mgogoro wa Yemen.