Sep 16, 2024 12:02 UTC
  • HAMAS yataka kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa Palestina

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ametoa wito wa kuundwa kwa serikali ya "muafaka wa kitaifa" kwa ajili ya kusimamia masuala ya Wapalestina.

Sami Abu Zuhri, mwanachama mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS nje ya nchi amesema hayo leo Jumatatu katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar na kuongeza kuwa, serikali hiyo ya umoja inapasa "ijumuishe makundi yote ya Wapalestina," na kusimamia masuala ya Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu.

Zuhri ameeleza bayana kuwa, "Hatukubali ubaguzi wowote kati ya Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na tunafanya hima [kufanikisha uundwaji wa] utawala jumuishi wa maeneo yote mawili na makundi ya Wapalestina."

Amesema HAMAS itakuwa ikishauriana na wawakilishi wa makundi mengine ya Palestina wakati wa mazungumzo yanayosubiriwa katika mji mkuu wa Misri, Cairo, kuhusu namna ya kusimamiwa Gaza baada ya kumalizika vita vinavyoendelea vya utawala wa Israel dhidi ya eneo hilo lililozingirwa.

Januari mwaka huu, utawala wa Kizayuni ulipendekeza uongozi wa Gaza ukabidhiwe kwa "makundi ya Palestina" ambayo hayakutajwa, huku ukiipa Tel Aviv udhibiti wa usalama wa eneo hilo. HAMAS hata hivyo, imekataa kata kata pendekezo hilo.

Hivi karibuni, makundi ya Wapalestina zikiwemo harakati za HAMAS na Fat'h zilifikia mwafaka wa kuyaunganisha makundi ya Palestina na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

 

Tags