Picha za satelaiti zaonyesha makombora ya Iran yalivyoharibu kambi ya anga ya F-35 ya Israel
(last modified Thu, 03 Oct 2024 12:37:23 GMT )
Oct 03, 2024 12:37 UTC
  • Picha za satelaiti zaonyesha makombora ya Iran yalivyoharibu kambi ya anga ya F-35 ya Israel

Picha za satelaiti za kambi muhimu ya jeshi la anga la utawala Israel iliyosheheni ndege za kivita za F-35 zinazotengenezwa Marekani zinaonyesha shimo kubwa kwenye paa baada ya Iran kuvurumisha makombora ya balistiki dhidi ya ngome za kijeshi za utawala huo ghasibu.

Iran siku ya Jumanne jioni ilivurumisha makombora 200 ya balistiki ambayo yalilenga kambi za kijeshi na kijasusi za utawala wa Kizayuni wa Israel katika shambulio la kulipiza kisasi, lililopewa jina la Operesheni Ahadi ya Kweli II.

Operesheni hiyo iliyosubiriwa kwa hamu na watu wengi ilikuja kujibu mauaji ya utawala wa Kizayuni dhidi ya mkuu wa Hamas Ismail Haniya katika mji mkuu wa Iran Tehran, Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrallah na kamanda wa IRGC Abbas Nilforoushan, mshauri wa kijeshi wa Iran nchini Lebanon, katika mji mkuu wa Lebanon wa Beirut.

Ripoti ya shirika la habari la AP siku ya Jumatano ilionyesha picha za satelaiti za uwanja wa ndege  za kivita wa Nevatim kusini mwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel, zikionyesha uharibifu mkubwa kwenye paa la majengo kadhaa karibu na njia kuu ya kurukia ndege, huku mabaki ya maeneo yaliyobomolewa yakiwa yametapakaa katika eneo hilo.

Kituo cha Jeshi la Anga cha Nevatim husheheni ndege za kivita za Israel zikiwemo zile za kisasa kabisa za F-35 Lightning II zinazozalishwa nchini Marekani.

Kituo hiki kikubwa cha anga chenye njia nne za kuruka na kutua ndege kiko katika eneo la takriban kilomita za mraba 50 katika jangwa la Negev, kilomita 15 mashariki mwa Beersheba na kilomita 12 kaskazini mwa Dimona.

Hapo kuna vikosi vitatu vya ndege za kivita za F-35 zilizotengenezwa Marekani pamoja na ndege za usafiri za C-130, ndege za Boeing 707 za kusheheni mafuta ya ndege za kivita na ndege nyingine za upelelezi.

Angalau video saba tofauti zimeonyesha makombora 20 hadi 30 ya Iran yakilenga uwanja huo ambayo yalisababisha uharibifu mkubwa na kulingana na vyanzo vingine, makombora hayo ya Iran yameharibu ndege  20 za F-35

Mapema jana, Waziri wa Ulinzi wa Iran, Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh alithibitisha kuwa operesheni hiyo ya makombora ilikuwa na mafanikio katika kiwango cha zaidi ya asilimia 90.