Mamia ya misikiti imebomolewa na Israel katika Ukanda wa Gaza
Wizara ya Wakfu ya Gaza imetangaza kuwa misikiti zaidi ya 800 imebomolewa kikamilifu katika Ukanda wa Gaza huko Palestina kufuatia vita na mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kidini ya Palestina imetangaza katika taarifa yake kuwa, jeshi la Kizayuni limebomoa kikamilifu misikiti 814 ya Ukanda wa Gaza katika kipindi cha mwaka mmoja wa uchokozi na vita vya mauaji ya halaiki dhidi ya Ukanda huo.
Aidha kwa mujibu wa tangazo hilo, makombora na mashambulizi ya anga ya utawala ghasibu wa Israel yamebabisha uharibifu mdogo pia kwa misikiti zaidi ya 200 katika eneo hilo.
Taarifa ya Wizara ya Wakfu ya Gaza imeendelea kubainisha kuwa utawala ghasibu wa Israel umelenga makaburi zaidi ya 60, kufukua na kuiba miili ya mashahidi na wafu zaidi ya elfu moja.
Vilevile utawala ghasibu wa Israel umeharibu makao 15 ya Wizara ya Wakfu yakiwemo makao makuu ya wizara hiyo, makao makuu ya Radio Qur'ani, Ofisi ya usimamizi wa Wakfu huko Khan Yunis na kituo cha kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu cha wizara hiyo; ambapo hadi sasa wafanyakazi 91 wa wizara hiyo pia wameuawa shahidi.
Aidha hujuma hizo za Israel dhidi ya Gaza zimeripotiwa kulenga ofisi za kamati za kukusanya zaka, madrasa za Qurani na makao makuu ya Benki ya Wakfu.