Sheikh Qassim: Hakuna shaka Hizbullah itamshinda adui Mzayuni
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amepongeza Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa iliyofanywa na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS na makundi mengine ya mapambano yenye makao yao makuu huko Gaza dhidi ya utawala ghasibu wa Israel na kusema kuwa, operesheni hiyo iliashiria mwanzo wa kubadilisha taswira ya eneo la Asia Magharibi kwa kuyahusisha makundi ya Muqawama.
Sheikh Naim Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema hayo katika hotuba aliyoitoa kwa mnasaba wa kutimia mwaka mmoja wa Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa na kusisitiza kuwa, harakati hiyo imejiandaa kikamilifu kukabiliana na mashambulio ya utawala haramu wa Israel.
Amebainisha kuwa, mrengo wa Muqawama nchini Lebanon utaendeleza njia ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah kwa nguvu zake zote na kusisitiza kuwa, "Hakuna shaka tutaushinda utawala mtenda jinai za Israel."
Katika hatua nyingine, Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetangaza kuwa imeshambulia kwa maroketi 85 mji wa bandari wa Haifa unaokaliwa kwa mabavu na Israel, kikiwemo kitongoji cha Kiryat Motzkin.
Shirika la habari la IRNA, likinukuu vyombo vya habari vya Muqawama limeripoti kuwa, mashambulizi ya makombora ya usiku wa kuamkia leo yameupelekea utawala wa Kizayuni kuamsha ving'ora mjini Tel Aviv na Galilaya (Galilee) na maeneo yanayoizunguka miji hiyo miwili.
Sauti za ving'ora pia zilisikika huko Masqaf, al-Mutla katika eneo la Isba al-Jalil, kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.