HAMAS na Fat'h wakutana Cairo na kufikia makubaliano mazuri kuhusu Ghaza
(last modified Mon, 04 Nov 2024 02:25:20 GMT )
Nov 04, 2024 02:25 UTC
  • HAMAS na Fat'h wakutana Cairo na kufikia makubaliano mazuri kuhusu Ghaza

Vyombo mbalimbali vya habari vilitangaza jana Jumapili kwamba, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na ile ya Fat'h zimekutana mjini Cairo Misri na kufikia maamuzi mazuri kuhusu Ghaza baada ya vita.

Afisa mmoja wa Misri amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, ujumbe wa Fat'h umeonana na ujumbe wa HAMAS na pande mbili zimetilia mkazo mno suala la kuwa na kauli moja makundi yote ya Palestina kuhusu Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Afisa huyo wa Misri ambaye hakutaka kutajwa jina lake ameiambia televisheni ya al Qahira kwamba Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina atatoa hukumu ya kuundwa kamati kuu ambayo itakuwa na jukumu la kuendesha masuala ya Ukanda wa Ghaza baada ya vita. Kamati hiyo itaundwa na wasomi wa kada mbalimbali wa Kipalestina. Kabla ya hapo gazeti la al Arabi al Jadid lilikuwa limetangaza kuwa HAMAS imekubaliana na pendekezo hilo. 

Khalil al Hayya

 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kamati hiyo itasimamia ujenzi mpya wa Ukanda wa Ghaza. Harakati za Fat'h na HAMAS, zimepongeza pia juhudi zinazofanywa na Misri zilizopelekea kuitishwa kikao hicho na kufikiwa makubaliano hayo.

Kabla ya hapo, timu moja ya HAMAS iliyoongozwa na Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati hiyo, Khalil al Hayya pamoja na mkuu wa masuala ya kisiasa ya Ukanda wa Ghaza, Basem Naim ilielekea mjini Cairo Misri kufanya mazungumzo kuhusu kile kilichoitwa: "siku ya kabla ya kusimamishwa jinai za Israel kwenye Ukanda wa Ghaza."