PNGO yakosoa marufuku ya Israel ya kupelekwa misaada ya kibinadamu Gaza
(last modified Thu, 07 Nov 2024 02:31:35 GMT )
Nov 07, 2024 02:31 UTC
  • PNGO yakosoa marufuku ya Israel ya kupelekwa misaada ya kibinadamu Gaza

Amjad Shawa ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Palestina (PNGO) amekosoa vikali hatua ya kinyama ya utawala haramu wa Israel ya kupiga marufuku upelekaji wa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Dkt. Shawa amesema kuwa, kuongezeka kwa mzozo wa kibinadamu na kushadidi kwa njaa ya wakaazi wa Gaza kunatokana na kuzidishwa kwa vizuizi vya njia ya misaada ya kuingia katika Ukanda wa Gaza.

Mkurugenzi huyo wa Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Palestina (PNGO) ameeleza kuwa, wavamizi wa Israel wameweka vizuizi vikali vya kuingia kwa misaada huko Gaza, haswa kaskazini mwa eneo hilo, ili kuzidisha njaa kwa wakazi wake.

Radiamali hiyo inafuatia hatua ya Bunge la Kizayuni (Knesset) kupasisha mswada wa kupiga marufuku shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada na Kazi kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) ambalo ni mojawapo ya mashirika makubwa ya kutoa misaada katika Ukanda wa Gaza, likiwa na wafanyakazi wapatao 13,000 ambao wamekuwa wakifanya kazi wakati wote wa vita huko Gaza.