HAMAS: Mwafaka umefikiwa kuhusu Wapalestina 620 ambao Israel ilichelewesha kuwaachia huru
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema, ujumbe wake umehitimisha ziara yake katika mji mkuu wa Misri Cairo na umefikia makubaliano na wapatanishi ya kutatuliwa ucheleweshaji uliofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuwaachilia huru wafungwa Wapalestina ambao ilipasa waachiliwe siku ya Jumamosi iliyopita kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya pande hizo mbili.
"Iwapo hakutatokea mabadiliko ya dakika za mwisho, mabaki ya mateka wanne Wasirael yatarejeshwa Jumatano usiku bila ya hafla rasmi, na wafungwa wa Kipalestina wataachiliwa hatua kwa hatua kutoka kwenye jela za Israel," ameongeza afisa huyo wa Kizayuni.
Awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha vita huko Ghaza ilianza Januari 19, ikihusisha hatua tatu za utekelezaji, ambazo kila moja ilipangiwa kuchukua muda wa siku 42, huku mazungumzo ya awamu inayofuata yakitakiwa kuanza kabla ya kukamilika awamu ya sasa.
Ikiwa ni sehemu ya awamu hii, ambayo inahusisha kuachiliwa mateka 33 Waisrael, wakijumuishwa walio hai na waliokufa, makundi ya Muqawama ya Palestina tayari yamewaachia huru mateka 25 walio hai na miili ya mateka wanne waliofariki katika nyakati saba tofauti.
Utawala wa Kizayuni wa Israel kwa upande wake, hadi sasa umechelewesha kuachiliwa huru wafungwa wapatao 620 wa Kipalestina, licha ya Hamas kutekeleza kikamilifu ahadi zake chini ya makubaliano hayo.../