Wanawake wa Palestina wanalishwa futari zilizooza kwenye jela za Israel
(last modified Tue, 11 Mar 2025 11:35:40 GMT )
Mar 11, 2025 11:35 UTC
  • Wanawake wa Palestina wanalishwa futari zilizooza kwenye jela za Israel

Mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa kidhulma katika jela za Israel ikiwemo ile jela ya Damon wanaishi katika mateso makubwa yasiyoelezeka hasa ndani ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani ikiwa ni pamoja na kulazimishwa kula vyakula vilivyooza wakati wa futari na kutangaziwa nyakati sizo za wakati wa daku na futari.

Hayo yameripotiwa na Shirika la Habari la Shahab la Palestina ambalo limeandika katika ripoti yake kwamba, Kamati ya Masuala ya Mateka na Wapalestina Walioachiwa Huru imeripoti kuwwa wanawake wa Palestina wanapitia mateso na unyanyasaji mkubwa katika jela ya Damon wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mateka wa kike wa Kipalestina waliwaambia mawakili wa Shirika la Palestina la Masuala ya Mateka na Walioachiliwa Huru kwamba askari magereza wa Israel wanatangaza saa za uwongo za kufungua na kuanza saumu wakati wa Ramadhani lakini baya zaidi ni kwamba wanawapa chakula kilichooza.

Taasisi hiyo ya mateka wa Palestina imesema: "Karmel Khawaja, msichana wa Kipalestina mwenye umri wa miaka kumi na tisa na amekuwa gerezani tangu Machi 2, 2025, analalamikia hali mbaya ya jela na uhaba mkubwa wa nguo kwa mateka wanaoshikiliwa kwenye jela hiyo."

Kwa mujibu wa shirika hilo, mateka mwengine Mpalestina, Bi Fida Assaf mwenye umri wa miaka 49 mkaazi wa Qalqilya, anaugua saratani ya damu na hajapata matibabu yoyote hadi hivi sasa, hajapelekwa hospitalini wala kupewa dawa angalau za kumpunguzia maumivu tangu alipotekwa nyara na wanajeshi wa Israel wiki mbili zilizopita.

Jana, Riyad al-Ashqar, mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Mateka wa Kipalestina alisema: "Mateka wa kike wananyimwa haki za kimsingi kabisa za maisha yao. Wazayuni wanawanyanyasa vibaya Wapalestina hao. Wanawahamisha kwa makusudi kutoka seli hadi seli nyingine kwa shabaha ya kuwanyanyasa na kuwakosesha utulivu.