HAMAS haitokwama kwa kuuliwa shahidi viongozi wake
Kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas amesema kuwa, عtawala wa Kizayuni unajidanganya unapodhani kwamba utaweza kuiangamiza Hamas kwa kuwaua shahidi makamanda wake.
Pars Today imemnukuu Sami Abu Zuhri, Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya Hamas nje ya Palestina akisema: "Hamas ni harakati ya Muqawama ambayo ina mizizi imara huko Palestina, ina makamanda wengi, na haiiwezi kukwama kwa kuuliwa kigaidi makamanda wake."
Ameongeza kuwa: Utawala wa Kizayuni ulitumia fursa ya usitishaji vita kukusanya taarifa za siri kuhusu makamanda na viongozi wa Hamas ili ipate kuwaua kigaidi.
Lakini amesema: "Damu za viongozi na makamanda wa Hamas hazina rangi nyekundu zaidi kuliko damu za watoto na vijana wa Ghaza, na kwamba mauaji hayo hayatatuzuia kuendelea na njia ya mapambano."
Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya Hamas nje ya Palestina pia amesema: "Kinachotokea hivi sasa katika Ukanda wa Ghaza ni cha kutisha zaidi kuliko matukio ya miezi 15 iliyopita, kwani mauaji ya umati ya hadharani yanafanywa kila siku na Israel katika Ukanda wa Ghaza lakini hilo halitotuvunja moyo, tutaendelea na mapambano hadi ukombozi kamili."
Hii ni katika hali ambayo, wanajeshi wa utawala katili wa Kizayuni wa Israel wameendelea kufanya ukatili kwa kuwaua shahidi Wapalestina wengine 17 katika mashambulizi ya alfajiri ya leo Jumanne kwenye Ukanda wa Ghaza, ikiwa ni siku moja baada ya kuua shahidi Wapalestina zaidi ya 60 akiwemo ripota wa Al Jazeera, Hossam Shabat katika ukanda huo.