Ripota Maalumu wa UN: Hali ya kibinadamu Ghaza ni mbaya mno
(last modified Sat, 26 Apr 2025 11:09:58 GMT )
Apr 26, 2025 11:09 UTC
  • Ripota Maalumu wa UN: Hali ya kibinadamu Ghaza ni mbaya mno

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa amesema leo Jumamosi kwamba hali ya kibinadamu huko Ghaza ni mbaya sana.

Akihojiwa na televisheni ya Al Jazeera, afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, Israel imeharibu kwa makusudi miundombinu yote ya uzalishaji wa chakula huko Ghaza.

Ameongeza kuwa: "Ni wazi Israel inawaadhibu kwa njaa watu milioni 2.2 huko Ghaza, na vitendo hivi vimekuwa na taathira mbaya ya moja kwa moja na kali kwa maisha ya watu wa kawaida katika eneo hilo la Palestina."

Ripota huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Haki ya Chakula ameonya kuhusu kutokea janga kubwa la kibinadamu ikiwa jinai hizo za utawala wa Kizayuni zitaendelea, na ametoa mwito wa kuchukukliwa hatua za haraka na jamii ya kimataifa, za kukomesha mashambulizi na uharibifu unaofanywa na Israel.

Kwa upande wake shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, baraza la mawaziri la Israel limeidhinisha mswada wa kupiga marufuku kuingizwa misaada yoyote ya kibinadamu huko Ghaza licha ya kwamba Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu yameonya kuwa wananchi wa Ghaza wamo kwenye mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha vita vya kikatili vya pande zote dhidi ya ukanda huo, mwezi Oktoba 2023.

Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetangaza kuwa, hali ya watoto huko Ghaza ni mbaya sana na kwamba eneo hilo liko ukingoni mwa kuporomoka.