Jolani: Hay’at Tahrir al-Sham inafanya mazungumzo na Israel
Mkuu wa utawala wa Hay’at Tahrir al-Sham (HTS) unaoongoza nchini Syria amethibitisha habari ya kuwepo mazungumzo "yasiyo ya moja kwa moja" kati ya utawala huo na utawala wa Israel eti kwa lengo la kuzuia kile alichokiita mripuko usioweza kudhibitiwa wa hali ya mambo, wakati huu ambapo Tel Aviv inaendeleza uchokozi wa kijeshi usiokoma dhidi ya Syria.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron mjini Paris siku ya Jumatano, Abu Mohammed al-Jolani alisisitiza udharura wa kufanyika mazungumzo hayo ili kuepusha sinario, ya hali "kutoka nje ya udhibiti."
Kadhalika amesema serikali yake inafanya mawasiliano na nchi zenye uhusiano mzuri na utawala wa Israel ili kuzitaka nchi hizo ziiase Tel Aviv ikomeshe uchokozi wake dhidi ya Syria.
Aidha jana Jumatano, Reuters iliripoti kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu umeanzisha njia ya kufanikisha mazungumzo hayo yasiyo ya moja kwa moja baina ya serikali ya mpito ya Syria na Israel. Mwezi uliopita, Jolani alifanya ziara Imarati, ambayo ina uhusiano rasmi na Tel Aviv baada ya kusaini makubaliano ya upatanishi wa Marekani mnamo 2020.
Aliutaja uchokozi wa kijeshi wa utawala wa Tel Aviv dhidi ya Syria kuwa "ukiukaji" wa Makubaliano ya Mwaka 1974 kati ya Damascus na Tel Aviv. Mkataba huo ulitiwa saini baada ya Israel kunyakua eneo la Miinuko ya Golan ya Syria wakati wa vita vilivyoungwa mkono na nchi za Magharibi miaka saba iliyopita.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Jolani alisema yuko tayari kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel. Hayo ni kwa mujibu wa barua inayoripotiwa kuwa alimtumia Rais wa Marekani Donald Trump. Alidai kuwa Syria iko tayari kuanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia na Israel na kujiunga na Mkataba wa Abraham, lakini "kwa masharti sahihi".