Foreign Affairs: Dola bilioni 2 za Marekani zimeshindwa kuipigisha magoti Yemen
(last modified Sun, 11 May 2025 12:07:32 GMT )
May 11, 2025 12:07 UTC
  • Foreign Affairs: Dola bilioni 2 za Marekani zimeshindwa kuipigisha magoti Yemen

Jarida la makala za uchaguzi la Foreign Affairs limesisitiza kuwa licha ya rais wa Marekani, Donald Trump kudai kuwa Ansarullah ya Yemen imesalimu amri, lakini harakati hiyo haijaathiriwa na mashambulizi ya Marekani yaliyoitia hasara ya dola bilioni mbili nchi hiyo, na wanamapambano wa Yemen wanaendelea na mashambulizi yao dhidi ya Israel.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars; Jarida la Marekani la Foreign Affairs limekiri kwamba licha ya serikali ya Trump kutumia zaidi ya dola bilioni 2 kufanya mashambulizi dhidi ya Yemen, lakini imeshindwa kuipigisha magoti Ansarullah na kwamba ni Marekani ndiyo iliyolazimika kukubali kusitisha mapigano. Tarehe 6 mwezi huu wa Mei, rais wa Marekani alitangaza kuwa hatofanya tena mashambulizi nchini Yemen. 

Kabla ya hapo Trump alifanya mashambulizi dhidi ya nchi hiyo kwa kisingizio cha kukabiliana na vitisho vya wanajeshi wa Yemen katika Bahari Nyekundu na kulizuia jeshi la Yemen lisishambulie Israel. Mashambulizi ya Trump yameua idadi kubwa ya raia wa nchi Yemen.

Jarida la Foreign Affairs limesema kwenye makala yake hiyo ya kiuchambuzi kwamba viongozi wa Ansarullah sasa wanaweza kusema kwamba wamesimama kidete kukabiliana na mashambulizi ya Marekani na kupata ushindi mkubwa.

Aidha, Wayemen sasa wana muda zaidi wa kujikita katika kukabiliana na Israel. Wakati wa mashambulizi yake dhidi ya Yemen, Marekani inadai kuwa ililenga zaidi ya maeneo 1,000, ikiwa ni pamoja na viwanja vya ndege na miundombinu muhimu, lakini, kwa mujibu wa jarida la Marekani la Foreign Affairs, Washington imeshindwa kuzuia uwezo wa Ansarullah wa kushambulia maeneo ya utawala wa Kizayuni na kuzuia meli za Marekani na Israel kutumia Bahari Nyekundu. Limesema: uamuzi wa Trump wa kuomba suluhu na Ansarullah ni njia ya mkato ya kujitoa kwenye kinamasi cha Yemen.

Jarida hilo pia limesema: Hasara kubwa iliyopata Marekani katika vita vyake vya Yemen si tu imeongeza mashinikizo ya kifedha kwa Marekani bali pia imezusha wasiwasi miongoni mwa watunga sera wa Washington kwamba huenda Marekani ikaingizwa katika vita vingine visivyo na mwisho katika eneo la Mashariki ya Kati.