Yemen yayaonya mashirika ya ndege ya kimataifa kuhusu safari za kuelekea Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion wa Israel
Afisa wa ngazi ya juu wa Yemen ameyatahadharisha mashirika ya ndege ya kimataifa juu ya kuanza tena safari za kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ben Gurion katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) huku operesheni za kulipiza kisasi za nchi hiyo ya Kiarabu zikiendelea.
Afisa huyo wa Yemen ambaye jina lake halikutajwa ameiambia televisheni ya al Mayadeen kwamba makampuni yanayotoa huduma za usafiri wa anga na yanayotaka kuanzisha safari zake kuelekea viwanja vya ndege vya Israel yanapasa kubadili njia zao na kuzingatia kwa makini tahadhari zinazotolewa na jeshi la Yemen.
Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Yemen amesisitiza kuwa jeshi la nchi hiyo linaendelea kutekeleza mzingiro wa anga dhidi ya Israel, na si tu kwa kushambulia uwanja wa ndege wa Ben Gurion pekee wa utawala huo ghasibu.
Ameongeza kuwa: Urushaji wa makombora na droni za Yemen kuelekea uwanja wa ndege wa Ben Gurion na katika taasisi nyingine za Israel unatekelezwa kwa kasi inayoongezeka na si kwa bahati mbaya.
Vikosi vya Ulinzi vya Yemen na taifa zima kwa ujumla hawatishwi na vita vya kisaikolojia na wako jadi kukabiliana na hatua zozote za kuwaweka chini ya mashinikizo au kudhoofisha kampeni yao dhidi ya Israel', ameongeza afisa wa ngazi ya juu wa Yemen alipozungumza na televisheni ya al Mayadeen.