Msalaba Mwekundu: Mfumo wa afya wa Gaza 'ni dhaifu mno'
Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imeonya kuwa, mfumo wa huduma za afya katika Ukanda wa Gaza ni "dhaifu sana" wakati huu ambapo vita vya Israel vinaendelea katika eneo hilo lililozingirwa.
Shirika hilo limesema katika taarifa kwamba, hospitali za eneo hilo zinahitaji ulinzi wa haraka na kuimarishwa wakati huu ambapo Israel inaendelea kushambulia na kulizingira eneo hilo.
Taarifa ya ICRC imeongeza kuwa, mfumo huo unakabiliwa na mashinikizo yanayoongezeka kutokana na kuongezeka kwa viwango vya majeruhi wa mashambulizi ya Israel katika vituo vya misaada.
Mamia ya Wapalestina wameuawa shahidi katika hujuma za Israel karibu na maeneo ya kusambaza misaada yanayoendeshwa na Wakfu wa Kibinadamu wa Gaza (GHF) unaoungwa mkono na Marekani na Israel tangu ulipozinduliwa Mei 27. Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Serikali ya Gaza iliripoti jana Jumapili kwamba, idadi ya waliouawa katika maeneo ya misaada ya GHF imeongezeka hadi 125. Wengine 736 wanaripotiwa kujeruhiwa, huku tisa wakitoweka wasijulikane walipo.
Hii ni katika hali ambayo, Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, Francesca Albanese ameieleza operesheni ya GHF "vazi la kibinadamu" na "mbinu ya mauaji haya ya kimbari".
Amesema maeneo ya kusambazia misaada huko Gaza yamegeuka na kuwa 'machinjio ya binadamu' huku utawala Israel ukiendeleza mashambulizi ya kinyama.
Mashirika ya UN, yakiashiria kwamba mpango wa Marekani na Israel wa kusambaza misaada huko Gaza una hatari kubwa, yamesisitiza kuwa: Gaza imekuwa Jahanamu ya kweli, na sasa njaa inatishia maisha ya watoto wasiopungua 71,000.
Mashirika hayo kwa mara nyingine tena yamekariri wito wao wa kusitishwa vita na hujuma za kijeshi katika Ukanda wa Gaza na kukomesha mzingiro wa kikatili dhidi ya ukanda huo.