Makampuni ya kigeni yanaukimbia utawala wa Kizayuni wa Israel
Makampuni ya kigeni yaliyokuwa na uwekezaji huko Israel (Palestina inayoikaliwa kwa mabavu) yameendelea kukimbia kutoka huko kutokana na kukosekana usalama wa kibiashara.
Vyombo vya habari vya lugha ya Kiebrania vinaripoti kuhusu kukimbia kwa makampuni ya kigeni ambayo yalikuwa yakifanya kazi huko Israeli kabla ya vita.
Tovuti ya habari ya gazeti la kiuchumi la Marker inaripoti kuwa, kampuni ya Marekani iliyokuwa ikifanya kazi Israel kwa miaka mitano ikiwa na mtaji wa dola milioni 100 imefunga shughuli zake na kukimbia kutoka Isreal sambamba kuwafuta kazi wafanyakazi wake wote.
Ripoti hiyo, iliyochapishwa katika chombo cha habari cha lugha ya Kiebrania, inasisitiza kwamba John Graham, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Marekani ya Seekwell, aliwafahamisha wafanyakazi wa kampuni hiyo kuhusu suala hili katika siku za hivi karibuni na akatangaza kwamba, kuanzia sasa, shughuli zote za kampuni hiyo zitafanywa nchini Marekani na kwamba, kama italazimu idadi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo watahamishiwa Marekani, huku wengine watapoteza kazi yao kuanzia mwezi ujao.
Kwa mujibu wa duru za habari, wafanyakazi wa kampuni hiyo wanasisitiza kuwa wote wamefukuzwa kazi, na kwamba wale ambao watahamishiwa Marekani watakuwa kwa muda mfupi na maalumu, na watakwenda huko tu kuhamisha uzoefu, na watafutwa kazi na kampuni hiyo mara baada ya kuhamisha uzoefu wao.
Mazingira katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel yanazidi kuwa hatarishi kutokana na mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani (drone) yanayofanywa na Jeshi la Yemen kama sehemu ya kisasi dhidi ya kampeni inayoendelea ya mauaji ya kimbari inayotekelezwa na Tel Aviv katika Ukanda wa Gaza.