Wapinzani wa Netanyahu wazidi kumshinikiza aondoke madarakani
Mashinikizo ya vuguvugu la upinzani katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina (Israel) ya kutaka kumpindua Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na baraza lake la mawaziri yameongezeka.
Mashinikizo hayo sasa yanaonekana kushika kasi na kufanya Netanyahu anayekabiliwa na kashfa nyingi za ufisadi kukalia kuti kavu.
Netanyahu anakabiliwa na shutuma kali kutoka kwa familia za mateka wa Israel. Familia hizo zinamnyooshea kidole cha lawama kwa kushindwa kufikia makubaliano ya kumaliza vita na kubadilishana mateka na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS. Familia hizo zinasisitiza kwamba shinikizo la kijeshi kwa Ukanda wa Gaza litasababisha tu vifo vya mateka hao, na sio kuachiliwa kwao huru.
Wazayuni walikusanyika mbele ya makao makuu ya chama tawala cha Likud katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu dhidi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na utendaji wa baraza lake la mawaziri wakitaka kufikiwe makubaliano ya kubadilishana mateka na harakati ya Hamas.
Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth liliripoti jana Jumatatu kwamba familia za wafungwa wa Kizayuni na baadhi ya wanaharakati wengine zilifanya maandamano na kukusanyika mbele ya makao makuu ya chama cha Likud mjini Tel Aviv. Washiriki wa maandamnao hayo walisikika wakitoa nara dhidi ya Netanyahu na kutoa mwito wa kufikiwa haraka iwezekanavyo makubaliano ya kubadilishana mateka.
Wapinzani wa Netanyahu hasa familia za mateka ambao ndugu zao wanashikiliwa na HAMAS wanasema kuwa, kuendelea vita hakuna natija ghairi ya kuongeza masaibu na machungu kwa pande zote mbili.