Israel yaua Wapalestina 60 ndani ya saa 24 zilizopita huko Ghaza
(last modified Tue, 10 Jun 2025 07:40:34 GMT )
Jun 10, 2025 07:40 UTC
  • Israel yaua Wapalestina 60 ndani ya saa 24 zilizopita huko Ghaza

Mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Ghaza yamesababisha vifo vya Wapalestina 60 ndani ya saa 24 zilizopita, Hayo ni kwa mujibu wa duru za afya za ukanda huo.

Mashambulizi ya Israel yamelenga maeneo mengi na kuzidisha mzozo wa kibinadamu katika eneo hilo.

Katika mji wa Ghaza, madaktari watatu Wapalestina na wengine wawili wameuawa shahidi katika shambulio la anga kwenye kitongoji cha Shuja'iyya na wengine kadhaa kujeruhiwa. Wanajeshi wa Israel wameshambulia eneo moja karibu na Hospitali ya al-Shifa, na kujeruhi watu wengi. Imeshambulia pia eneo la as-Saftawi, kaskazini mwa mji wa Ghaza na kusababisha hasara kwa raia.

Huko kusini mwa Ghaza pia, Wapalestina 13 waliokwenda kuchukua misaada katika eneo la usambazaji wa misaada lililotengwa na Israel na Marekani wameuawa shahidi huku wengine watatu wakiripotiwa kuuawa shahidi katika shambulio tofauti la anga karibu na hapo.

Tangu kuanza jinai za Israel za mauaji ya umati dhidi ya Wapalestina, hadi hivi sasa vifo vya Wapalestina vilivyothibitishwa ni 54,927 huko Ghaza, ingawa duru za afya zinasema kuwa, idadi halisi ya watu waliouawa shahidi ni kubwa zaidi. Wahanga wakubwa wa jinai hizo za Israel ni wanawake, watoto wadogo na wazee.

Hayo yanajiri katika hali ambayo Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imeonya kuwa, mfumo wa huduma za afya kwenye Ukanda wa Ghaza ni "dhaifu sana" wakati huu ambapo jinai za kutisha za Israel zinaendelea katika eneo hilo lililozingirwa kila upande kwa miaka mingi.