Bidhaa za Israel zasusiwa katika maduka ya nchi za Ulaya
Maduka makubwa katika nchi kadhaa za Ulaya yameacha kuuza bidhaa za Israel ili kujibu ghadhabu za wanunuzi za bidhaa hizo kutokana na vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza.
Maduka hayo ya jumla nchini Uingereza, Italia, na Ujerumani - ikiwa ni pamoja na makampuni kama Co-op na Aldi - yameamua kusitisha uuzaji wa bidhaa za Israeli kutokana na hasira za watu juu ya uhalifu wa kivita wa Israel.
Ofer Levin, chanzo cha habari katika sekta ya kilimo cha Israel, ameliambia gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth kwamba, wazalishaji waliarifiwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuhusu kususiwa bidhaa zao katika nchi za Ulaya, na maelezo rasmi yakitaja upatikanaji wa bidhaa mpya za ndani-lakini sababu ya kweli ni ya kisiasa.
Ususiaji huo ulioanzishwa na watu kwa bidhaa za Israel unafanyika katika nchi hizo zinazounga mkono moja kwa moja vita vya utawala wa Israel dhidi ya Gaza.
Tangu kuanza kwa uvamizi wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, idadi ya vifo imeongezeka hadi zaidi ya 57,000, kulingana na mamlaka ya afya ya eneo hilo.
Huku mauaji ya kimbari yakiwa yanaendelea kufanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wa Gaza, nchi nyingi duniani zinaendelea kujiunga na kampeni ya kususia bidhaa za Israel na vilevile za makampuni mengi ya Kimarekani yanayouunga mkono utawala huo wa kibaguzi.