Kiongozi mkuu wa PKK, Abdullah Ocalan: Hatudai tena uhuru wa Kurdistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128154-kiongozi_mkuu_wa_pkk_abdullah_ocalan_hatudai_tena_uhuru_wa_kurdistan
Abdullah Ocalan, Kiongozi aliyefungwa gerezani wa Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan (PKK) amewahutubia wafuasi wake kupitia ujumbe wa video kwa mara ya kwanza baada ya miongo kadhaa akiwaambia kwamba mapambano ya silaha dhidi ya Uturuki yamekwisha na kwamba sasa ni wakati wa kuhamia kwenye siasa za kidemokrasia.
(last modified 2025-10-15T09:12:33+00:00 )
Jul 10, 2025 12:45 UTC
  • Kiongozi mkuu wa PKK, Abdullah Ocalan: Hatudai tena uhuru wa Kurdistan

Abdullah Ocalan, Kiongozi aliyefungwa gerezani wa Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan (PKK) amewahutubia wafuasi wake kupitia ujumbe wa video kwa mara ya kwanza baada ya miongo kadhaa akiwaambia kwamba mapambano ya silaha dhidi ya Uturuki yamekwisha na kwamba sasa ni wakati wa kuhamia kwenye siasa za kidemokrasia.

Ocalan, ambaye katika taarifa yake iliyoandikwa Februari alitaka kundi alilolianzisha livunjwe, amesema kwenye video hiyo mpya kwamba bunge la Uturuki inapasa liunde tume ya kusimamia upokonyaji silaha na kuchukua hatua za kusimamia mchakato wa amani.

Baada ya kuendesha vita dhidi ya Uturuki kwa muda wa miaka 40 iliyopita, PKK ilikubali kujivunja mwezi Mei kufuatia amri ya Ocalan.

"Vuguvugu la PKK, ambalo lilianzishwa katika kukabiliana na kunyimwa [utambulisho wa Wakurdi] na kutafuta taifa tofauti, sasa limemalizika, pamoja na mkakati wake wa ukombozi wa kitaifa," ameeleza Ocalan kuhitimishwa ajenda ya kujitenga iliyokuwa ikipiganiwa na kundi hilo.

"Kuwepo kwa Wakurdi kumetambuliwa, na kwa hivyo, lengo letu kuu limefikiwa", amesema kiongozi huyo wa PKK aliyeko gerezani.

Ocalan ametangaza msimamo huo kabla ya hafla rasmi iliyopangwa kufanyika Ijumaa hii katika eneo la Sulaymaniyah nchini Iraq ambapo kundi moja la wapiganaji wa PKK na afisa wake mwandamizi wanatarajiwa kuweka silaha chini kiishara.../