Syria na Israel zafikia makubaliano tete ya usitishaji vita
Rais wa mpito wa Syria na waziri mkuu wa Israel wamekubaliana kusitisha mapigano kufuatia makabiliano ya umwagaji damu ya siku kadhaa katika Jimbo la Suweida, lililoko kusini mwa Syria.
Mjumbe Maalumu wa Marekani nchini Syria na balozi wake nchini Uturuki Tom Barrack ametangaza kuwa, Rais wa mpito wa Syria, Ahmed al-Sharaa na Waziri Mkuu wa utawala wa Israel Benjamin Netanyahu wamekubaliana kusitisha vita kufuatia mapigano katika Jimbo la Suweida, kusini mwa Syria,
Jimbo hilo limeripotiwa kuungwa mkono na Uturuki, Jordan, na mataifa mengine jirani, kwa mujibu wa mtandao wa telisheni ya wa Al-Mayadeen.
Barrack amehimiza makundi yote ya kidini na kikabila, ikiwa ni pamoja na Druze, Mabedui, na Sunni, kuweka chini silaha zao na kushirikiana kwa ajili ya kuunda Syria moja iliyoungana.
Shirika linalojiita Syrian Observatory for Human Rights limeripoti kwamba, idadi ya vifo huko Suweida kabla ya kusitishwa mapigano hayo ilikuwa imeongezeka hadi watu 718.
Hata hivyo, Wizara ya Afya ya Syria imetangaza kuwa, watu 260 wamepoteza maisha huku 1,698 wakijeruhiwa katika mapigano hayo ya hivi karibuni.
Kabla ya hapo, Baraza Kuu la Fatwa la Syria lilitangaza kuwa, ni kinyume cha sheria kufanya jaribio lolote la kutaka usaidizi kutoka kwa utawala wa Israel, ili kuwadhuru raia na kuzusha mifarakano.
Pia limesisitiza kuwa, serikali ya Damascus ina wajibu wa kuwalinda watu wote, kukataza kulenga Wasyria kwa misingi ya madhehebu, na kuimarisha ulinzi na misaada kwa wanaodhulumiwa ndani ya nchi kwa mujibu wa sheria za Kiislamu.