Maandamano makubwa kupinga jinai za Israel huko Gaza yafanyika Sweden
Wauungaji mkono wa Palestina wameandamana Stockholm, mji mkuu wa Sweden kupinga mashambulizi yanayoendelea kufanywa na jeshi la Israel dhidi ya shule na hospitali za Ukanda wa Gaza.
Mamia ya waandamanaji walikusanyika jana katika maidani ya Odenplan mjini Stockholm na kisha kuelekea katika jengo la Bunge la Taifa la Sweden.
Washiriki katika maandamano hayo walikuwa wamebeba bendera za Palestina na mabango huku wakipiga nara kama " Israel inauwa watoto wa Gaza" na " Simamisha mauaji ya kimbari ya wananchi wa Palestina".
Mwanaharakati wa Kiswidi, Lasse Eriksson ameashiria mauaji makubwa ya kimbari yanayotekelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na kusema: "Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni hivi karibuni wa shirika moja la Sweden, asilimia 75 ya wananchi wa nchi hiyo wanapinga vitendo vya Israel huko Gaza, lakini hakuna chama chochote cha kisiasa katika Bunge la Sweden kinachopinga vikali jinai hizo."
Eriksson pia ametaka utawala wa Kizayuni uwekewe vikwazo na kufukuzwa balozi wa utawala huo huko Stockholm.
Katika upande mwingine, vyombo vya habari jana usiku vilitangaza kuwa maelfu ya wananchi wa Jordan jana waliandamana katika kitongoji cha al-Tufaylah kulaani mzingiro dhidi ya Gaza na hatua ya Israel ya kuwasababishia njaa wakazi wa ukanda huo.
Waandamanaji hao wametangaza kuwa wako tayari kikamilifu kushiriki kijeshi na kuwahami wakazi wa Gaza dhidi ya jinai za Israel.