Mossad na Shabak zapinga mpango wa kuikalia kwa mabavu Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i129344
Wakuu wa Shirika la Ujasusi la Israel (MOSSAD) na Idara ya Ujasusi wa Ndani Shin Bet (SHABAK) zimepinga mpango wa kuukalia kwa mabavu mji wa Gaza kutokana na taathira zake mbaya.
(last modified 2025-08-09T15:19:22+00:00 )
Aug 09, 2025 15:19 UTC
  • Mossad na Shabak zapinga mpango wa kuikalia kwa mabavu Gaza

Wakuu wa Shirika la Ujasusi la Israel (MOSSAD) na Idara ya Ujasusi wa Ndani Shin Bet (SHABAK) zimepinga mpango wa kuukalia kwa mabavu mji wa Gaza kutokana na taathira zake mbaya.

Gazeti la Israel la Yedioth Ahronoth limeandika kuwa, wakuu wote wa idara za usalama, katika kikao cha baraza la mawaziri la usalama na siasa lililofanyika Alhamisi usiku, walipinga au kuchukua msimamo wa tahadhari kuhusu mpango wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu wa kuukalia kwa mabavu Ukanda wa Gaza.

Kuhusiana na suala hili, Kanali 12 ya Televisheni  ya Israel imeripoti kuwa: Tzachi Hanegbi, Mshauri wa Baraza la Usalama la Israel amepinga mpango wa Netanyahu kuhusu Gaza wakati wa mkutano wa baraza la mawaziri la utawala huo. 

Hanegbi aliliambia Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni kwamba: "Siko tayari kukata tamaa katika kuwanusuru mateka wa Israel. Ninakubaliana kabisa na Mkuu wa Majeshi kwamba kukaliwa kwa mabavu Gaza City kutahatarisha maisha yao, kwa hivyo napinga pendekezo la Waziri Mkuu." 

Eyal Zamir, Mkuu wa Majeshi ya Israel pia amepinga kukaliwa kwa mabavu Ukanda wa Gaza katika kikao cha baraza la mawaziri na kusema kwamba: Kukaliwa kwa mabavu na kuangamizwa eneo hilo kutachukua kati ya mwaka mmoja hadi miwili.