Mpango wa kuipokonya silaha Hizbullah, kosa la kimkakati kwa serikali ya Lebanon
Waziri wa Habari wa Lebanon, Paul Morcos amesisitiza katika hotuba yake kwamba: "Baraza la mawaziri la serikali limeidhinisha kubakisha silaha mikononi mwa majeshi ya serikali tu na kutumwa jeshi kusini mwa nchi."
Suala la kupokonywa silaha harakati ya Hizbullah nchini Lebanon ni mpango wa Marekani uliotwishwa kwa serikali ya Beirut. Mpango huo uliwasilishwa na Tom Barak, mjumbe wa kikanda wa Rais wa Marekani, Donald Trump. Kwa mujibu wa mpango huo wa hatua nne, Hizbullah inapaswa kupokonywa silaha ifikapo mwisho wa 2025.
Katika hatua ya kwanza, serikali ya Lebanon lazima itoe amri rasmi ndani ya siku 15 ya kujitolea kuipokonya silaha kabisa Hizbullah ifikapo Disemba 31, 2025. Wakati huo huo, Israel lazima ikomeshe shughuli zote za kijeshi za nchi kavu, angani na baharini. Katika awamu ya pili, ndani ya siku 60 tangu kuanza kwa mpango huo, serikali ya Lebanon inapaswa kuanza kutekeleza mpango wa upokonyaji silaha na kuwasilisha mpango wa kupeleka jeshi kudhibiti kikamilifu silaha za Hizbullah. Katika awamu ya tatu, ambayo itakuwa siku 90 baada ya kuanza mpango huo, Israel lazima ikamilishe kuondoka katika maeneo mawili inayoyakalia kwa mabavu. Katika hatua ya nne ya mpango huo wa Kimarekani, baada ya siku ya 120, silaha nzito zilizosalia za Hizbullah, zikiwemo ndege zisizo na rubani na mifumo ya makombora, lazima ziharibiwe au zikabidhiwe.
Hatua ya serikali ya Lebanon ya kukubali mpango huo imetambuliwa kuwa ni kosa la kistratijia kwa sababu kadhaa.
Kosa la kwanza ni kutokana na imani ya serikali ya Lebanon kwa utawala haramu wa Israel. Kwa mujibu wa mpango huu, Israel lazima isimamishe mashambulizi dhidi ya Lebanon na kuondoa katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Lebanon. Hata hivyo uzoefu wa kihistoria unaonyesha kuwa, utawala unaoikalia Quds kwa mabavu hautarudi nyuma kutoka kwenye maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, wala hautasimamisha mashambulizi. Hivyo kuitaka Hizbullah ikabidhi silaha zake wakati mvamizi akiwa bado nyumbani kwake ni sawa na kumtaka kundoo ajisalimishe kwa fisi katili na mvamizi.

Kosa lingine ni kuiamini Marekani. Serikali ya Marekani imeahidi kuuokoa uchumi wa Lebanon na kuifanya nchi yenye ustawi na utulivu mkabala wa kupokonywa silaha za Hizbullah. Marekani pia ilitoa ahadi kama hiyo kwa serikali za Iraq na Syria, lakini leo hii inaendelea kupora mapato ya mafuta ya Iraq; na huko Syria, sio tu kwamba hakuna dalili ya ustawi wa kiuchumi, lakini pia imeuruhusu utawala wa Kizayuni wa Isarel kushambulia Syria na kudhoofisha serikali ya Jolani.
Kosa jingine muhimu ni kwamba vikosi vya harakati ya Hizbullah ndio mhimili wa usalama wa Lebanon. Kutokana na juhudi za vikosi vya Hizbullah, eneo la kusini mwa Lebanon lilikombolewa kutoka kwa utawala wa Kizayuni mwaka 2000 na tangu mwaka 2006 hadi 2023 Israel halikuweza kutekeleza operesheni za kijeshi dhidi ya Lebanon kwa muda wa miaka 17. Kuipokonya silaha Hizbullah hakutaimarisha jeshi la Lebanon, kinyume chake, kunaweza kudhoofisha zaidi mamlaka ya nchi hiyo.
Kosa jingine muhimu ni kwamba, Hizbullah ina uungwaji mkono mkubwa wa watu nchini Lebanon. Kwa sasa viti vingi katika Bunge la Lebanon vinashikiliwa na Muungano wa Muqawama. Wananchi wa Lebanon wanapinga dhana ya kupokonywa silaha za Hizbullah, na msisitizo wa aina yoyote wa kutaka kutekekelizwa suala hilo unaweza kusababisha mipigano ya ndani nchini Lebanon. Kuhusiana na suala hilo mamia ya wananchi wa Lebanon walifanya maandamano katika mikoa mbalimbali ya nchi hiyo mapema Ijumaa kupinga uamuzi huo wa serikali ya Lebanon.

Nukta ya mwisho ni kwamba, uamuzi wa serikali ya Lebanon wa kutaka kuipokonya silaha Hizbullah unaweza kuzidisha migawanyiko ya kisiasa nchini humo na hata kuibia tena mapigano ya umwagaji damu ya mwaka 2008. Kuhusiana na suala hilo, mawaziri wa harakati mbili za Amal na Hizbullah, waliondoka kwenye kikao cha serikali ya Lebanon kuonyesha upinzani wao dhidi ya mpango huo wa Marekani na Wazayuni.
Kundi la Wafa lenye mafungamano na Hizbullah ya Lebanon lilitoa taarifa likisema: "Baadhi ya wanasiasa wanafuata amri za nchi za kigeni na wamesalimu amri kwa mashinikizo ya Marekani. Hawajali maslahi makuu ya nchi na umoja wa ndani."