Israel yamtia mbaroni mwakilishi wa UN Ukanda wa Ghaza
Utawala wa Kizayuni umemtia mbaroni mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika Ukanda wa Ghaza kwa tuhuma za kuwa na ushirikiano na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas.
Wahid Abdallah al Bursh amekuwa akifanya kazi katika Ukanda wa Ghaza katika Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP tangu mwaka 2013.
Duru za habari za Israel zimearifu kuwa Shirika la Intelijensia la utawala huo (Shabak) limesema kuwa kushiriki katika kuzikarabati nyumba za wanachama wa Hamas na kushirikiana katika masuala ya intelijensia na wanamapambano wa Palestina ni moja ya sababu zilizopelekea kutiwa nguvuni Wahid al Bursh.
Wakati huo huo Adnan Abu Husna mwakilishi wa ngazi ya juu wa Shirka la Utoaji Misaada ya Kibinadamu la Umoja wa Mataifa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu UNRWA ametahadharisha kuhusu hali mbaya ya kibinadamu huko Ukanda wa Ghaza na kueleza kuwa asilimia 80 ya wakazi wa eneo hilo wanahitaji misaada ya kibinadamu kukidhi mahitaji yao ya kimsingi. Utawala wa Kizayuni umezidisha mzingiro wake huko Ghaza tangu mwaka 2007 huku ukizuia pia kuingizwa bidhaa muhimu za mahitaji kama mafuta,dawa na vifaa vya ujenzi katika eneo hilo lililoathiriwa na vita.