WHO: Zaidi ya watu 15,600 wakiwemo watoto 3,800 wanahitaji kuondolewa haraka Gaza kwa ajili ya matibabu
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ameeleza kuwa watu zaidi ya 15,600 katika Ukanda wa Gaza, wakiwemo watoto 3,800, wanahitaji kuondolewa haraka katika eneo hilo lililokumbwa na vita ili kupata huduma maalumu ya matibabu.
Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus ameashiria mgogoro wa binadamu unaoendelea Ukanda wa Gaza ambako Israel inatekeleza kampeni ya mauaji ya kimbari na kuwasababishia njaa wakazi wa eneo hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO amesisitiza kuwa, wagonjwa wengi wanaendelea kukosa huduma muhimu za dharura na ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuruhusu kuingizwa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo.
Dr. Tedros amekariri wito wake akitaka kutekeleza makubaliano ya kusimamisha vita huko Gaza ili kuwezesha usambazaji wa misaada muhimu ya kibindamu na kuepusha majeruhi zaidi.
Wakati huo huo afisa wa ngazi ya juu kutoka Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) ameeleza kuwa hali ya mambo huko Gaza ni zaidi ya "maafa", kwa sababu eneo hilo halima mfumo wa afya unaofanya kazi.
Mohammed Abu Mughaiseeb ambaye ni Naibu Mratibu wa Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka huko Gaza amesema kuwa hali ya Gaza ni zaidi ya maafa. "Hali ni mbaya sana na haiwezi kuelekezeka kwa maneno; Ni hali ya majanga."
Ameongeza kuwa: "Sekta ya afya ya Ukanda wa Gaza imesambaratishwa na kuharibiwa kwa mpangilio maalumu kutokana na vita na mauaji ya kimbari ya Israel yanayoendelea kwa miezi 22 sasa, na hivyo kusababisha uharibifu wa hospitali nyingi za eneo hilo."