HAMAS: Pendekezo la Marekani halilengi kumaliza vita vya Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130604-hamas_pendekezo_la_marekani_halilengi_kumaliza_vita_vya_ghaza
Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, Bassem Naim amesema, mapendekezo ya awali yaliyowasilishwa na Marekani lengo lake lilikuwa ni kutaka yakataliwe, na si kuweza kufikiwa makubaliano ya kumaliza vita, kuhakikisha vikosi vamizi vinaondoka kikamilifu huko Ghaza na kutekelezwa mabadilishano ya wafungwa.
(last modified 2025-09-09T11:04:58+00:00 )
Sep 09, 2025 11:04 UTC
  • HAMAS: Pendekezo la Marekani halilengi kumaliza vita vya Ghaza

Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, Bassem Naim amesema, mapendekezo ya awali yaliyowasilishwa na Marekani lengo lake lilikuwa ni kutaka yakataliwe, na si kuweza kufikiwa makubaliano ya kumaliza vita, kuhakikisha vikosi vamizi vinaondoka kikamilifu huko Ghaza na kutekelezwa mabadilishano ya wafungwa.

Katika taarifa aliyotuma kwa shirika la habari la Quds Press, Naim ameeleza kwamba, pendekezo hilo la Marekani linapendekeza kupokelewa wafungwa wote katika siku ya kwanza, kufungamanisha kuondoka kwa jeshi la Israel na kuundwa kwa serikali inayokubalika na utawala huo sambamba na kukabidhiwa majukumu ya kiusalama. Pendekezo hilo aidha linajumuisha utoaji tafsiri mpya kuhusu Hamas, kuzingatia msamaha kwa wanachama wake, na kupokonywa silaha Muqawama "bila kutajwa suala la ujenzi upya" wa Ghaza.

Afisa huyo wa Hamas amesisitiza kuwa harakati hiyo na makundi mengine ya Muqawama yanafuatilia "makubaliano ambayo yatasimamisha vita na mauaji ya kimbari, na kufungua njia ya kupatikana suluhu ya kisiasa inayokidhi malengo halali ya kitaifa."

Mapema jana Jumatatu, Rais wa Marekani Donald Trump alisema, 'Waisraeli wamekubali masharti ya pendekezo lake la uwezekano wa kubadilishana wafungwa na kusitisha mapigano huko Ghaza, na sasa ni zamu ya Hamas kukubali".

Kadhalika, Trump alizungumzia uwezekano wa "kufikiwa karibuni hivi makubaliano ya kumaliza vita dhidi ya Ghaza kulingana na moja ya mapendekezo," akiashiria pia kile alichokiita "onyo la mwisho" kwa Hamas kuhusu matokeo hasi ya kulikataa pendekezo jipya.../