Kikao cha dharura cha mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kufanyika Qatar kujadili mashambulio ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130694-kikao_cha_dharura_cha_mataifa_ya_kiarabu_na_kiislamu_kufanyika_qatar_kujadili_mashambulio_ya_israel
Mji mkuu wa Qatar Doha utakuwa mwenyeji wa mkutano wa dharura wa kilele wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu Jumapili na Jumatatu ijayo kuchunguza mashambulizi ya Wazayuni dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu yaliyolenga makao ya viongozi wa HAMAS.
(last modified 2025-09-12T03:21:16+00:00 )
Sep 12, 2025 03:21 UTC
  • Kikao cha dharura cha mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kufanyika Qatar kujadili mashambulio ya Israel

Mji mkuu wa Qatar Doha utakuwa mwenyeji wa mkutano wa dharura wa kilele wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu Jumapili na Jumatatu ijayo kuchunguza mashambulizi ya Wazayuni dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu yaliyolenga makao ya viongozi wa HAMAS.

Kwa mujibu wa Al Jazeera, Doha, mji mkuu wa Qatar, utakuwa mwenyeji wa mkutano wa dharura wa nchi za Kiarabu na Kiislamu siku ya Jumapili na Jumatatu wiki ijayo kujadili mashambulizi ya Israel dhidi ya Doha.

Ajenda kuu ya mkutano huu imetajwa kuwa ni kujadili shambulio la hivi majuzi la Israel dhidi ya Qatar.

Sambamba na kutangaza kuufanyika mkutano huo, Qatar imetangaza kuwa, ina haki ya kujibu jinai hiyo ya Israel huko Doha iliyowalenga viongozi waandamizi wa HAMAS.

Taarifa zinasema kuwa, Qatar imezungumza na timu yake ya wanasheria juu ya namna ya kumuwajibisha Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kwa kuhusika na uvunjaji wa sheria za kimataifa.

Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari, waziri mkuu wa Qatar ameelezea shambulizi hilo kama "kitendo cha ugaidi wa kiserikali kilichofanywa chini ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu" na "ukiukaji wa uhuru".

"Nchi ya Qatar ina haki ya kujibu mashambulizi ya Israel na itachukua hatua madhubuti dhidi ya ukiukaji wowote wa kizembe au uchokozi unaotishia usalama wake na utulivu wa kikanda," taarifa imesema.

Imeongeza kuwa wanaahidi kuchukua "hatua zote muhimu kujibu". Imeendelea kusema kuwa "Qatar itaanza mapitio ya kina ya sera na taratibu za kuzuia vitendo hivyo na kuzuia kujirudia."