Familia za mateka: Netanyahu ndiye kikwazo cha kuwarudisha mateka nyumbani
Familia za mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kwa mara nyingine tena zimemtuhumu Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel kuwa kikwazo cha kufikiwa makubaliano ya kuachiliwa ndugu zao.
Familia hizo sambamba na kuandamana zimesema Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ndiye "kikwazo kimoja" kinachozuia kurejea ndugu zao na kufikia makubaliano ya amani.
Jukwaa la Mateka na Familia Zilizotoweka: Warudisheni Nyumbani Sasa liliandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba mashambuliz ya Israel dhidi ya Qatar wiki iliyopita yanaonyesha "kila wakati mpango unapokaribia, Netanyahu anauhujumu".
Matamshi ya kundi hilo yamekuja baada ya Israel kufanya mashambulizi dhidi ya viongozi wakuu wa Hamas katika mji mkuu wa Qatar wa Doha, ambapo Hamas ilisema iliua wanachama wake watano na afisa wa usalama wa Qatar.
Siku ya Jumamosi, Netanyahu alisema kuwaondoa viongozi wa Hamas nchini Qatar "kutaondoa kikwazo kikuu" cha kuwaachilia mateka na kumaliza vita.
Pia aliishutumu Hamas kwa kuzuia majaribio yote ya kusitisha mapigano ili kuondoa vita huko Gaza.
Hivi sasa Netanyahu anaandamwa na mashinikizo makubwa ya ndani yanayomtaka afikie makubaliano na HAMAS ya kubadilishana mateka. Baadhi ya familia ambazo ndugu zao wanashikiliwa zinaamini kwamba, Netanyahu ndiye kikwazo na kwamba, kila mara kunapokaribia kufikiwa makubaliano basi hukwamisha hilo kwa visingizo na tuhuma zisizo na msingi au kwa kufanya mashambulio dhidi ya Hamas.