Russia: Hatutashiriki kwenye mpango wa Trump kuhusu Gaza
Sambamba na kusisitizia utayarifu wa Russia wa kutatua mgogoro wa Asia Magharibi, Msemaji wa Ikulu ya Russia (Kremlin) amesisitiza kuwa Moscow haitashiriki katika mpango wa Rais wa Marekani juu ya Ukanda wa Gaza.
Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov aliuambia mkutano na waandishi wa habari, akijibu swali kuhusu mpango huo wa Trump wa Gaza kwamba, "Russia daima inaunga mkono na kukaribisha juhudi zozote zinazolenga kuzuia maafa ambayo yanatokea kwa sasa (huko Gaza)."
Hata hivyo amekanusha ushiriki wa Russia katika mpango wa Trump, akisema Moscow haijapokea taarifa zozote kutoka Washington katika suala hilo.
"Tunatumai mpango huu utatekelezwa, ili usaidie kutatua mzozo wa Mashariki ya Kati kwa njia ya amani," Peskov amesema, akiongeza kuwa Russia inadumisha mawasiliano na pande zote kwenye mzozo na iko tayari kuwezesha suluhisho la amani ikilazimu, Shirika la Habar la Anadolu liliripoti.
Siku ya Jumatatu, Rais wa Marekani, Donald Trump alitamka mbele ya waandishi wa habari akiwa pamoja na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kwamba, eti amekaribia sana kutatua mgogoro wa Palestina na kudai kuwa kile alichokiita mpango mpya wa amani wa Washington haujabuniwa kusimamisha vita tu huko Gaza lakini pia eti kujenga amani ya kudumu katika Mashariki ya Kati.
Mpango huo wa Trump umekosolewa vikali na duru mbali mbali za kieneo na kimataifa, ikiwemo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas na Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina.
Hamas imepinga mpango huo ikieleza kuwa hauna jipya wala dhamana yoyote ya kutekelezwa, na kusisitiza kuwa mpango huo hauna maana yoyote.