Wasiwasi wa kimataifa kuhusu hali ya wafungwa wa Kipalestina
Katika kuendelea wasiwasi wa kimataifa kuhusu hali mbaya ya wafungwa wa Kipalestina wanaoendelea kuteseka katika jela za utawala wa kibaguzi wa Israel, Shirika la Msamaha Duniani sawa na mashirika mengine eti ya kutetea haki za binadamu ya nchi za Magharibi ambayo kwa kawaida hunyamazia kimya jinai za Israel dhidi ya raia wa Palestina, mara hii limeutaka utawala huo umuachie huru Bilal Kayed mfungwa wa Kipalestina ambaye amegoma kula chakula tangu miezi miwili iliyopita.
Bilal Kayed amegoma kula chakula akilalamikia kuendelea kufungwa na utawala huo bila ya kufunguliwa mashtaka. Bilal Kayed alitiwa mbaroni mwishoni mwa mwaka 2001 na mwaka 2002, mahakama ya kijeshi ya Israel ilimhukumu kifungo cha miaka 14 jela kwa tuhuma za kujihusisha na shughuli za harakati ya Popular Front for the Liberation of Palestine. Kayed alitazamiwa kuachiwa huru katikati ya mwezi Juni mwaka huu, hata hivyo Israel imeamua kuendelea kumfunga jela bila ya kumfungulia mashtaka. Kifungo hicho ni kifungo cha jela ambapo mfungwa hushikiliwa gerezani bila ya kufikishwa mahakamani na bila ya kukabiliwa na tuhuma ambapo viongozi wa Israel huruhusu kufungwa jela raia wa Palestina hadi miezi sita; na kifungo hicho kinaweza kurefushwa kwa kipindi chochote kile. Kwa utaratibu huo, wafungwa wa Kipalestina wanafungwa na kuteseka katika jela za Israel bila ya kukabiliwa na tuhuma au kufunguliwa mashtaka.
Kuongezeka hatua za utawala wa Kizayuni za kuwakatia vifungo vya muda mrefu jela wafungwa wa Kipalestina na kurefusha muda wa sheria zilizo dhidi ya ubinadamu zinazohusiana na wafungwa hao wanaofungwa bila kufunguliwa mashtaka, ni jambo linaloweza kutathminiwa katika fremu ya vitendo vya Israel vya kukataa kuwaachia huru wafungwa wa Palestina walioko katika jela za utawala huo.
Hii ni katika hali ambayo takwimu na ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa katika miezi kadhaa ya hivi karibuni wafungwa wa Palestina walioko katika jela za utawala wa Kizayuni wameendelea kukabiliwa na hali mbaya. Kuhusiana na suala hilo, klabu ya wafungwa wa Kipalestina huko nyuma ilitangaza kuwa wafungwa 1000 wa Kipalestina katika jela za Israel wanaugua maradhi mbalimbali; huku karibu 160 kati yao wakiugua maradhi ya saratani na magonjwa mengine sugu. Klabu hiyo imesema wafungwa hao wanaogua wana hali mbaya ya kiafya na wanahitaji matibabu ya haraka.
Idadi ya wafungwa wa Kipalestina walioko katika jela za Israel wamefikia elfu saba kutokana na siasa zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya raia wa Palestina; huku takwimu zikionyesha kuwa wafungwa wengi wamepata maradhi yasiyotibika. Utawala wa Kizayuni unashadidisha jinai zake dhidi ya raia wa Palestina na kukwepa kutekeleza maazimio ya kimataifa likiwemo azimo la Geneva linalohusu wafungwa wa Kipalestina.
Kwa njia hiyo, utawala wa Kizayuni unatekeleza miamala yoyote inayotaka iwe ni ya kibaguzi au ya kimabavu dhidi ya raia wa Palestina. Na kwa msingi huo Wapalestina wengi wanaokamatwa na Israel huwa na hatima isiyojulikana, wengi wao huaga dunia katika jela za utawala huo au kupata ulemavu wa kudumu na maradhi yasiyoweza kutibika.