Lazzarini: Kujenga upya shule za Gaza ndio kipaumbele
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i132304-lazzarini_kujenga_upya_shule_za_gaza_ndio_kipaumbele
Philippe Lazzarini, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), amesema kuwa, kurejesha haki ya elimu kwa watoto wa Gaza ni jambo la dharura na muhimu zaidi baada ya kusitishwa mapigano.
(last modified 2025-10-23T05:45:52+00:00 )
Oct 23, 2025 02:40 UTC
  • Lazzarini: Kujenga upya shule za Gaza ndio kipaumbele

Philippe Lazzarini, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), amesema kuwa, kurejesha haki ya elimu kwa watoto wa Gaza ni jambo la dharura na muhimu zaidi baada ya kusitishwa mapigano.

Amesema, elimu haiwezi kusubiri, kwa sababu kukata tamaa ni adui mkubwa wa watoto huko Gaza.

Lazzarini amesema kuwa watoto wa Gaza wamenyimwa kikatili haki yao ya elimu na wanahangaika na umaskini, kuhama makazi yao, na kiwewe kikubwa cha kisaikolojia kilichosababishwa na vita.

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) amesema kuwa, shule nyingi katika Ukanda wa Gaza imma zimeharibiwa au zimevunjwa kabisa na zinahitaji ujenzi wa haraka ili kuanza tena masomo.

Aliongeza: Hivi sasa, watoto wapatao 60,000 wameweza kuendelea na masomo yao katika maeneo ya muda ya elimu ndani ya kambi za wakimbizi, na zaidi ya watoto wengine 300,000 wanapata masomo ya msingi kupitia mawasiliano yaIntaneti internet kwa msaada wa walimu wa UNRWA.

Kwa mujibu wa Lazzarini, zaidi ya walimu 8,000 wako tayari kuanza tena kufundisha punde tu hali inapokuwa sawa.

Aidha ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua haraka iwezekanavyo kujenga upya shule, kutoa mahema, na mavazi ya majira ya baridi kwa watoto wa Gaza, kwa sababu mustakabali wa Gaza unaanzia madarasani na sio katika magofu ya vita.

Ripoti rasmi zinasema, mashambulizi ya utawala ghasibu wa Israel yameharibu asilimia 97 ya shule za Ukanda wa Gaza na hivyo kuhatarisha mustakbali wa kielimu wa wanafunzi laki tatu wa Kipalestina katika eneo hilo.