UAE, mnunuzi wa siri katika mkataba mkubwa wa silaha na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i134502-uae_mnunuzi_wa_siri_katika_mkataba_mkubwa_wa_silaha_na_israel
Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umetambuliwa kama mnunuzi 'asiyejulikana' kwenye mkataba wa dola bilioni 2.3 uliosainiwa mwezi uliopita na kampuni za kuzalisha silaha ya Israel ya Elbit Systems, ripoti inasema.
(last modified 2025-12-20T02:34:55+00:00 )
Dec 20, 2025 02:34 UTC
  • UAE, mnunuzi wa siri katika mkataba mkubwa wa silaha na Israel
    UAE, mnunuzi wa siri katika mkataba mkubwa wa silaha na Israel

Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umetambuliwa kama mnunuzi 'asiyejulikana' kwenye mkataba wa dola bilioni 2.3 uliosainiwa mwezi uliopita na kampuni za kuzalisha silaha ya Israel ya Elbit Systems, ripoti inasema.

Ripoti ya Intelligence Online, iliyotolewa Alkhamisi imesema kwamba, makubaliano ya dola bilioni 2.3 kati ya Abu Dhabi na Tel Aviv yanahusisha utoaji wa mifumo ya kijeshi ya hali ya juu kwa zaidi ya miaka minane.

Kwa mujibu wa duru hizo, makubaliano hayo ni miongoni mwa mfululizo wa mauzo makubwa ya silaha na makampuni ya silaha ya Israel katika miaka ya hivi karibuni. Hapo awali Elbit alitangaza mkataba huo bila kutaja taifa linalonunua au kufichua mifumo ya silaha inayohusika.

Kufichuliwa kwa UAE kama mteja wa siri wa Elbit kunakuja huku kukiwa na lawama kubwa kutoka kwa mashirika ya haki za binadamu kuhusu mauaji ya halaiki ya Israel katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa.

Mashirika ya kimataifa kama vile Oxfam yameonya kwamba, ununuzi na uuzaji wa mifumo ya kijeshi ya hali ya juu unahatarisha ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na madhara zaidi kwa raia.

Haya yanajiri huku Waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu akitangaza kuwa, serikali yake imeidhinisha makubaliano makubwa ya uuzaji wa gesi asilia kwa Misri yenye thamani ya karibu dola bilioni 35, akielezea kwamba makubaliano hayo ni makubwa zaidi katika historia ya Israel kwa upande wa thamani na ujazo wa usafirishaji nje.