Saudia yaendelea kushambulia maeneo ya mamluki wa Imarati nchini Yemen
-
Saudia yaendelea kushambulia maeneo ya mamluki wa Imarati nchini Yemen
Ndege za kivita za Saudi Arabia zimeendelea kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya mamluki wa Imarati yakiwemo makao makuu ya mamluki hao huko mashariki mwa Yemen.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, ndege za kivita za Saudi Arabia kwa mara nyingine zimeshambulia maeneo ya Baraza la Mpito la Kusini ambalo ni la mamluki wa Muungano wa Falme za Kiarabu yaani Imarati.
Vyanzo vya habari vimetangaza kwamba mashambulizi hayo ya anga yamepiga makao makuu ya mamluki wa Imarati huko Al-Ghaiza, mji ambao uko katikati mwa mkoa wa Al-Mahra.
Siku chache zilizopita pia, ndege za kivita za Saudi Arabia zilishambulia shehena za silaha zilizopelekwa na Imarati huko Yemen ambazo zilitakiwa kuwafikia wapiganaji wa Baraza la Mpito la Kusini.
Baada ya hapo Wizara ya Ulinzi ya Imarati ilitangaza kwamba imeamua kujiondoa kijeshi nchini Yemen baada ya ndege za kivita za Saudia kushambulia mamluki wake kwenye bandani ya Mukalla ya Yemen.
Lakini Baraza la Mpito la mamluki wa Imarati limepinga hatua hiyo ya Abu Dhabi na kusema kuwa, mashambulizi ya ndege za kijeshi za Saudia katika mji wa bandari wa Mukalla ni uvamizi na ni uchokozi rasmi dhidi ya Yemen.
Wataalamu wanasema kuwa, matukio hatari yanaendelea kutokea nchini Yemen hivi sasa, hasa baada ya ugomvi kati ya Riyadh na Abu Dhabi kugeuka kutoka migogoro ya kimya kimya na kuwa mapambano ya wazi ya kisiasa na kijeshi, ambayo hatimaye yamepelekea ndege za Saudia kushambulia maeneo ya mamluki wa Imarati huko Yemen.