Wazayuni wamefanya mashambulizi 24,000 katika Ukingo wa Magharibi
Ripoti ya kila mwaka ya shirika moja la Palestina imefichua kuwa, katika kipindi cha mwaka uliopita wa 2025, Wazayuni wamefanya karibu mashambulizi 24,000 katika eneo la Ukingo wa Magharibi la Mto Jordan huko Palestina.
Ripoti ya kila mwaka ya shirika la Palestina linaloitwa "Kukabiliana na Ukuta wa Utengano na Makazi" katika eneo la Ukingo wa Magharibi inaonesha kuwa, jeshi la Israel na walowezi wa Kizayuni wamefanya mashambulizi 23,827 dhidi ya raia wa Palestina na mali zao katika majimbo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi mwaka 2025. Hiyo ni idadi kubwa mno ya mashambulizi yaliyowahi kurekodiwa katika kipindi mwaka mmoja.
Jinai hizo zinajumuisha mashambulizi 1,382 dhidi ya ardhi na mazao ya kilimo, mashambulizi 16,664 dhidi ya watu binafsi, na mashambulizi 5,398 dhidi ya mali. Walowezi wa Kizayuni wamehusika katika mashambulizi 4,723 kati ya hayo.
Mashambulizi hayo yamepelekea pia kuhamishwa kwa nguvu makundi 13 ya jamii za Wabedouin wa Kipalestina, yakijumuisha familia 197 za Wapalestina hao.
Sehemu nyingine ya ripoti hiyo inasema kwamba vitendo 538 vya ubomoaji wa majengo vilifanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wavamizi wa Kizayuni wameteka karibu asilimia 41 ya eneo lote la Ukingo wa Magharibi na wameimarisha udhibiti wao kwa asilimia 70 wa eneo hilo.
Ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni unaendelea kulaaniwa kote duniani. Mahakama ya Kimataifa ya Haki pia imesisitizia uharamu wa vitongoji hivyo vya walowezi wa Kizayuni.