UNRWA: Misaada inayoingia Gaza inakabiliwa na vivingiti shadidi vya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i135284-unrwa_misaada_inayoingia_gaza_inakabiliwa_na_vivingiti_shadidi_vya_israel
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi Wapalestina (UNRWA) limetangaza kuwa vizingiti vilivyowekwa na  jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika njia za kuingia Ukanda wa Gaza vimesababisha kupungua kwa kiwango kikubwa misaada kwa  Wapalestina katika eneo hilo.
(last modified 2026-01-09T11:00:54+00:00 )
Jan 09, 2026 11:00 UTC
  • UNRWA: Misaada inayoingia Gaza inakabiliwa na vivingiti shadidi vya Israel

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi Wapalestina (UNRWA) limetangaza kuwa vizingiti vilivyowekwa na  jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika njia za kuingia Ukanda wa Gaza vimesababisha kupungua kwa kiwango kikubwa misaada kwa  Wapalestina katika eneo hilo.

Katika taarifa, UNRWA imetangaza kuwa jeshi la utawala wa Kizayuni lingali linakalia nusu ya Ukanda wa Gaza na hata limevuka mstari wa njano.

Taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imelalamika kuwa Israel imezuia au kupiga marufuku misaada ya kibinadamu kuwafikia Wapalestina wanaoteseka katika  Ukanda wa Gaza.

Hayo yanajiri wakati ambao Wizara ya Afya ya Palestina imeeleza katika takwimu zake za hivi karibuni kwamba, Wapalestina zaidi ya 71,000 wameuawa shahidi katika vita vya mauaji ya kimbari vilivyoanzishwa na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza Oktoba 2023.

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imesema watu wasiopungua 4 wameuawa shahidi na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika muda wa saa 48 zilizopita huku Gaza, na kufanya idadi ya mashahidi wa mashambulizi hayo ya kinyama kufikia 71,395.

Ofisi Kuu ya Takwimu ya Palestina ilisema katika ripoti yake ya kufunga mwaka wa 2025 kwamba, mauaji ya kimbari, watu kulazimishwa kuhama makazi yao, na uharibifu mkubwa wa miundombinu muhimu, yote haya yamesababisha maafa makubwa na ya muda mrefu kwa utulivu wa kijamii, hali ya kiuchumi na kijamii na haki za binadamu katika ardhi za Palestina.

Ofisi Kuu ya Takwimu ya Palestina kwa upande wake imeripoti kuwa, Wapalestina zaidi ya 72,000 wameuawa shahidi tangu kuanza vita na mauaji ya kimbari ya Israel Oktoba 7, 2023 ambapo asilimia 98 ya vifo vimesajiliwa huko Gaza. Kiwango hicho kimetajwa kuwa kikubwa sana kuwahi kushuhudiwa katika historia ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Wapalestina. 

Hadi mwishoni mwa mwaka uliomalizika wa 2025, idadi ya Wapalestina ilikuwa karibu milioni 5.56, milioni 3.43 walikuwa wakazi wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na milioni 2.13 huko Gaza.

Nayo Ofisi ya Habari ya Ukanda wa Gaza imesema kuwa, uchokozi unaoendelea kufanywa na utawala ghasibu wa Israel wa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano hadi sasa umepelekea kuuawa shahidi Wapalestina wasiopungua 425, huku wengine 1,206 wakijeruhiwa.