Walowezi wanatumia watoto kusumbua jamii za Wapalestina Ukingo wa Magharibi
Walowezi wa Kizayuni mara kwa mara wanatumia vikundi vya watoto wa Kizayuni kuzisumbua na kuzifanyia maudhi jamii za Wapalestina na kuharibu maeneo yao ya kilimo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu na Wazayuni hao.
Gazeti la Kizayuni la Haaretz limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, walowezi wa Kizayuni wamepewa kazi maalumu ya kuzishambulia jamii za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi na kutoruhusu jamii hizo ziishi kwa utulivu na amani.
Matukio hayo ni sehemu ya kampeni kubwa ya kuwalazimisha Wapalestina kuhama makazi yao na katika kipindi cha hivi karibuni, wamewaondoa Wapalestina wengi kwenye maeneo yao na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.
Ripoti hiyo inaonesha kwamba walowezi wa Kizayuni mara kwa mara wanawatumia watoto hata wenye umri wa miaka 12, kuzisumbua jamii za Wapalestina wa vijijini.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, walowezi hao huwa wanafika kwa miguu, kwa matrekta au kwa kupanda ATV katika jamii za Wapalestina hao. Wanakusanyika kwa makundi katika maeneo ya Wapalestina na kuanza huharibu mali, huwatishia wakazi wa maeneo hayo na kuharibu maeneo yao ya mashambani vikiwemo vyanzo vya maji ambavyo ndilo tegemeo kuu la maisha ya jamii hizo za Wapalestina.
Ripoti hiyo ya Haaretz imeongeza kuwa, mara nyingi walowezi hao Wazayuni hubeba marungu, visu na silaha nyingine kuzishambulia jamii za Wapalestina. Ripoti hiyo imeongeza kwamba, matukio hayo hayatokei kwa bahati nasibu. Watoto Wazayuni wanazichosha jamii za Wapalestina kupitia unyanyasaji wa mara kwa mara wa kila wiki. Baada ya hapo walowezi watu wazima wenye silaha hufika na kuanza kuwashambulia Wapalestina hao na kuwalazimisha waache makazi yao.