Israel yashambuliwa kwa makombora kutoka Iran, Yemen na Hizbullah
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i137726-israel_yashambuliwa_kwa_makombora_kutoka_iran_yemen_na_hizbullah
Mashambulizi ya pamoja ya makombora kutoka Iran, harakati ya Hizbullah ya Lebnon na Jeshi la Yemen yamelenga ngome za utawala wa Kizayuni wa Israel mapema siku ya Jumatano.
(last modified 2026-04-01T07:11:32+00:00 )
Apr 01, 2026 04:35 UTC
  • Israel yashambuliwa kwa makombora kutoka Iran, Yemen na Hizbullah

Mashambulizi ya pamoja ya makombora kutoka Iran, harakati ya Hizbullah ya Lebnon na Jeshi la Yemen yamelenga ngome za utawala wa Kizayuni wa Israel mapema siku ya Jumatano.

Chaneli ya 13 ya Televisheni ya utawala wa Kizayuni wa Israel imenukulu Kamandi ya Ulinzi wa Ndani ikitangaza kuwa mara tu baada ya kuanza mashambulizi ya makombora kutoka Iran, mifumo ya tahadhari ya mapema iliwashwa katika mji wa Tel Aviv pamoja na makazi ya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi. Baada ya mashambulizi hayo, vyanzo vya habari viliripoti kusikika kwa milipuko kadhaa mikubwa katika jiji la Tel Aviv.

Mwandishi wa mtandao wa Al‑Araby wa Qatar amesema kuwa kufuatia athari za kombora lenye kile kinachoelezwa kama vichwa kadhaa vya mabomu, milipuko kadhaa ilisikika katika ngome za utawala ghasibu wa Israel. Aidha, ripoti zimethibitisha kuwa makombora kadhaa yalipiga eneo la “Gush Dan”, kitovu cha miji ya kati ya Israel baada ya kukwepa ngao za makombora za utawala huo.

Taarifa nyingine zimesemaa kuwa kombora moja lilipiga jengo katika mji wa Bnei Brak. Huduma za dharura za Israel ziliripoti kuwa watu 20 walijeruhiwa katika mashambulizi hayo. Kwa kawaida utawala wa Israel hubana habari na hautangazi idadi ya watu wanaoangamizwa vitani.

Redio ya Jeshi la Israel imesema wimbi jingine la mashambulizi ya makombora limetekelezwa katika eneo la Negev na Bahari ya Chumvi.

 

Sambamba na mashambulizi yanayohusishwa na Iran, harakati ya Hizbullah ya Lebanon pia ilifyatua makombora kadhaa kuelekea ngome za kijeshi za Israel kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Mtandao wa Al‑Mayadeen nao umeripoti kuwa kutokana na mashambulizi ya pamoja ya Iran na Hizbullah, ving’ora vya tahadhari vilisikika katika ngome za utawala ghasibu za Israel — kuanzia Galilaya kaskazini hadi Negev kusini.

Wakati huo huo, Jeshi la Yemen limetangaza kuwa limelenga kwa mafanikio maeneo muhimu kistratijia ya utawala ghasibu wa Israel kusini kusini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kwa kutumia kombora la balestiki.

Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa Jeshi la Yemen, amesema katika taarifa iliyotolewa Jumatano kuwa operesheni hiyo ni ya tatu ya kijeshi inayotekelezwa katika muktadha wa mapambano ya Jihadi takatifu dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa vikosi vya Yemen vililenga maeneo nyeti ya adui Muisraeli kusini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Hujuma hiyo imetekelezwa kwa kutumia makombora ya balestiki.

Katika tamko hilo pia imesitizwa kuwa operesheni hizo zinafanywa kwa kuunga mkono medani za “Muqawama” au mapambano ya Kiislamu huko Iran, Iraq, Lebanon na Palestina. Aidha amesema kuwa kuongezeka kwa mashambulizi, uhasama na uhalifu wa adui dhidi ya Lebanon, Iran, Iraq na Palestina kutapelekea kushadidi operesheni za Jeshi la Yemen.

Jenerali Saree ameongeza kuwa operesheni hizo bado zinaendelea na zitazidishwa hadi pale mashambulizi yatakaposimamishwa na mzingiro dhidi ya Gaza utakapoondolewa.