Wabahrain waendeleza maandamano kupinga udikteta
Wananchi wa Bahrain wameendeleza maandamano dhidi ya utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.
Maandamano yamefanyika katika kijiji cha Abu Saiba nje kidogo ya mji mkuu Manama ambapo waandamanaji wametaka mwanazuoni wa Kiislamu Sheikh Ali Salman na wafungwa wote wa kisiasa waachiliwe huru .
Machafuko yaliibuka katika kijiji cha Nuwaidrat ambapo askari wa serikali walitumia gesi ya kutoa machozi, ambazo inasemekana zina kemikali za sumu, kuwatawanya waandamanaji. Maandamano kama hayo dhidi ya utawala yamefanyika katika kisiwa cha Sitra na vijiji vya al-Markh, al-Daih, Karzakan na al-Musalla.
Waandamanaji walibeba mabango ya baadhi ya watu ambao wameuawa na vikosi vya serikali tokea mwamko wa Kiislamu uanze nchini humo mwaka 2011.
Wananchi wa Bahrain wamesisitiza kuwa wataendeleza maandamano yao hadi pale utawala utakaposikiliza matakwa yao ambayo ni pamoja na kumalizwa ubaguzi, kufanyika marekebisho katika mfumo wa utawala na kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa.