UN yataka Nabil Rajab aachiwe huru haraka na bila ya masharti
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i22063-un_yataka_nabil_rajab_aachiwe_huru_haraka_na_bila_ya_masharti
Umoja wa Mataifa umeutaka utawala wa Aal Khalifa umwachie huru haraka na bila ya masharti yoyote Nabil Rajab, mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Bahrain anayeshikiliwa kwenye jela ya utawala huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 24, 2016 12:10 UTC
  • UN yataka Nabil Rajab aachiwe huru haraka na bila ya masharti

Umoja wa Mataifa umeutaka utawala wa Aal Khalifa umwachie huru haraka na bila ya masharti yoyote Nabil Rajab, mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Bahrain anayeshikiliwa kwenye jela ya utawala huo.

Liz Throssel, msemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa wana wasiwasi mkubwa mno na mwenendo wa uendeshaji kesi inayomkabili Rajab.

Msemaji huyo wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa kauli hiyo baada ya maafisa wa utawala wa Bahrain kutangaza siku ya Alkhamisi kuwa Nabil Rajab anakabiliwa na tuhuma za "kusababisha madhara kwa maslahi" ya utawala wa Manama na wa nchi zingine za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kutokana na makala anayohusishwa nayo ambayo ilichapishwa kwenye gazeti la kifaransa la Le Monde.

Wabaharaini wakiandamana kutaka Nabil Rajab aachiwe huru

 

Makala hiyo imelaani kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh kwa jinai inazofanya dhidi ya binadamu na kuzikosoa pia nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kwa kuzembea kuzuia uenezaji wa idiolojia ya Uwahabi.

Nabil Rajab alitiwa nguvuni tarehe 13 Juni mwaka huu kutokana na kuukosoa utawala wa Bahrain wa Aal Khalifa kwa kushiriki kwenye uvamizi ulioongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen. Endapo atapatikana na hatia kwa sababu ya tuhuma hizo anaweza kuhukumiwakifungo cha miaka 15 jela.

Msemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa Rajab amekamatwa kwa sababu ya "kutumia haki yake ya kutoa maoni".

Liz Throssel

Tarehe 5 Septemba mwaka huu pia mwanaharakati huyo wa kutetea haki za binadamu wa Kibahraini mwenye umri wa miaka 52 alifunguliwa shtaka jingine la kueneza taarifa za uongo dhidi ya utawala wa Aal Khalifa, siku moja baada ya makala aliyoandika kuchapishwa kwenye gazeti la New York Times la nchini Marekani.

Tarehe 15 mwezi huu, mahakama ya Bahrain iliakhirisha kesi yake kwa mara ya tano na kutangaza kuwa atafikishwa tena mahakamani tarehe 28 ya mwezi huuhuu wa Desemba.../