Dec 26, 2016 07:14 UTC
  • Maulamaa wa Bahrain walaani uhusiano wa nchi yao na Israel

Maulamaa nchini Bahrain wamelaani juhudi za utawala wa nchi hiyo za kuweka uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mwandishi wa Radio Tehran amenukuu tamko lililotolewa na maulamaa wa nchi hiyo wakisema kuwa, kitendo cha utawala wa ukoo wa Aal Khalifa cha kujaribu kuweka uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ni cha kichochezi na ni usaliti kwa umma wa Kiislamu na Kiarabu.

Maulamaa hao wamesema kuwa, wananchi walio macho hawawezi kulaghaiwa na hila za kilaghai za tawala za kidikteta. Wamesema, tawala hizo za kidikteta zinakwenda kinyume na matakwa na misimamo ya wananchi, bali zinazingatia tu manufaa yao binafsi na tawala zao katika mkabala wa manufaa ya taifa na utambulisho wa kidini na kitaifa wa wananchi wao.

Nchi za Magharibi ikiwemo Uingereza, zimejizatiti vilivyo kijeshi nchini Bahrain

 

Maulamaa wa Bahrain wametoa tamko hilo baada ya kufichuliwa malengo ya njama chafu za watawala wa nchi hiyo za kutaka kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao mikono yake imejaa damu za Wapalestina wasio na hatia.

Nao muungano wa vijana wa Mapinduzi ya Februari 14 umetoa taarifa ya kulaani hatua ya utawala wa Aal Khalifa wa Bahran wa kujaribu kuweka uhusiano wa kawaida na Israel na kusema kuwa, huo ni udhalilishaji mkubwa na ni kitendo kinachokwenda kinyume na matakwa ya wananchi Waislamu wa Bahrain. Vijana hao wamesema, kitendo cha tawala za nchi za Kiarabu ikiwemo Bahrain cha kuweka uhusiano wa kawaida na Israel hakiwezi kufuta dhati ya kigaidi na kiuadui ya utawala wa Kizayuni.

Tags