'Israel yaendelea kupoteza uungaji mkono duniani'
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amesema ataangalia upya uhusiano wa utawala huo na Umoja wa Mataifa.
Benjamin Netanyahu ameyasema hayo kufuatia hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la kulaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi unaofanywa na utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina.
Profesa Anthony Hall, mhariri mkuu wa gazeti la American Herald Tribune ameiambia kanali ya televisheni ya Press TV kuwa azimio la kihistoria la Baraza la Usalama dhidi ya ujenzi wa vitongoji unaofanywa na Israel ni ujumbe unaoonyesha wazi kuwa utawala huo haramu unapoteza uungaji mkono kimataifa.
Hall amefafanua kwa kusema: "Nguvu hii kubwa haribifu ya Israel, mradi huu wa uchu wa Ubeberu unaendelea kuwadhalilisha Wapalestina na watu wa ulimwengu mzima. Lakini azimio hili limedhihirisha kwa uwazi kabisa kwamba Mayahudi wa dunia nzima na Israel pamoja na raia wake wanapaswa waizingatie nukta hii, kwamba ujenzi wao wa kionevu wa vitongoji na upanuzi wake katika ardhi za watu wengine haupati tena msukumo na uungaji mkono wa jamii ya kimataifa".
Siku ya Ijumaa iliyopita, katika hatua isiyo ya kawaida, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio la kulaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi zilizoghusubiwa za Palestina na kuutaka utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ukomeshe upanuzi wa vitongoji hivyo. Azimio hilo lilipasishwa na nchi 14 wanachama wa Baraza la Usalama huku Marekani ikiamua kwa mara ya kwanza kutotumia kura yake ya veto kuzuia kupitishwa azimio la kuilaani Israel katika baraza hilo…/