Maji yamfika shingoni Abubakar al-Baghdadi, ateua warithi wake
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i22888-maji_yamfika_shingoni_abubakar_al_baghdadi_ateua_warithi_wake
Kiongozi wa kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) Ibrahim al-Samarrai, maarufu kama Abubakr al-Baghdadi ameteua watu watatu ambao wanatazamiwa kuchukua nafasi yake.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 05, 2017 16:10 UTC
  • Maji yamfika shingoni Abubakar al-Baghdadi, ateua warithi wake

Kiongozi wa kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) Ibrahim al-Samarrai, maarufu kama Abubakr al-Baghdadi ameteua watu watatu ambao wanatazamiwa kuchukua nafasi yake.

Shirika la habari la al-Sumariya limeripoti kuwa, ingawaje kuzungumzia kadhia ya kurithi nafasi ya Baghdadi kulipigwa marufuku katika maeneo yanayodhibitiwa na kundi hilo la Daesh katika mkoa wa Nainawa nchini Iraq karibu na mpaka na Syria, lakini makamanda wa matakfiri hao katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakilizungumzia suala hilo wazi wazi na hata kubainisha kuwa tayari kiongozi huyo wa ISIS ameteua warithi wake.

Kwa mujibu wa shirika la Syrian Observatory for Human Rights lenye makao makuu yake mjini London, makamanda wa Daesh tangu mwezi uliopita wamekuwa wakifanya mikutano ya siri na mashauriano ya kina kuhusu ni nani anayefaa kumrithi Abubakar al-Baghdadi, haswa baada ya gaidi huyo kutoweka kwa wiki kadhaa.

Abubakar Baghdadi na mmoja wa wake zake

Duru za habari zimedokeza kuwa, makamanda waandamizi wa Daesh nchini Iraq wamewaita viongozi wengine wa kundi hilo la kitakfiri walioko mjini Raqqah nchini Syria na kamanda wa tawi la kijeshi la kundi hilo la Jeish al-Sham, ili wakutane katika sehemu ya siri nchini Iraq kwa ajili ya kujadili mustakabali wa kundi hilo.

Katika miezi ya hivi karibuni magaidi wa Daesh wamepata pigo kubwa sana katika nchi za Iraq na Syria ambapo wanajeshi wa nchi hizo wanaendelea kukomboa ardhi zilizokuwa zimetekwa na wakufurishaji hao.

Kuna habari za mgongano kuhusu alipo Baghdadi, baadhi ya duru za habari zikisema kuwa kiongozi huyo wa Daesh yuko mafichoni mjini Mosul nchini Iraq, na baadhi zikisema kuwa alionekana mara ya mwisho mwezi Novemba mwaka jana katika mji wa al-Baaj, yapata kilomita 157 kusini magharibi mwa Mosul.

Operesheni ya kukomboa mji wa Mosul nchini Iraq

Kwa sasa jeshi la Iraq limetangaza kukomboa asilimia 70 ya maeneo ya mashariki mwa mji wa Mosul, ambao ulikuwa chini ya udhibiti wa Daesh tangu mwaka 2014.