Malengo ya Uturuki ya kuendelea kukiuka haki ya kujitawala Iraq
Licha ya malalamiko ya kila mara na mashitaka ya serikali ya Iraq katika asasi za kieneo na kimataifa, bado Uturuki imekataa kuondoa askari wake kutoka kambi ya kijeshi ya Bashiqa.
Kwa mara nyingine Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Ibrahim al-Jaafari amesisitizia udharura wa kuondoka askari wa Uturuki kaskazini mwa nchi yake. Uturuki ilituma mamia ya askari wake katika kambi ya kijeshi ya Bashiqa mjini Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa (Nineve) mwishoni mwa mwaka 2015. Hatua hiyo ya Uturuki ambayo ni kinyume cha sheria, imefanywa kwa kisingizio cha kutoa mafunzo kwa wapiganaji wa Kikurdi wa Peshmerga na pia kukabiliana na magaidi.
Hatua hiyo ya Uturuki ni ukiukaji wa wazi wa haki ya kujitawala Iraq kwani imefanyika bila ya idhini ya Baghdad na ndio maana mara kadhaa viongozi wa Iraq wamekuwa wakisisitizia wajibu wa kuondoka askari hao wa kigeni kutoka ardhi ya Iraq. Katika kulalamikia hatua hiyo ya Uturuki, serikali ya Baghdad iliwasilisha mashitaka yake katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC). Mbali na hayo serikali ya Iraq pia ilipinga vikali kushiriki askari hao wa Uturuki katika operesheni za kuukomboa mji wa Mosul ambapo hadi sasa operesheni hizo zinaendelea kwa mafanikio makubwa. Awali serikali ya Ankara ilichukua hatua zilizoonesha wazi tabia yake ya kupenda kujitanua, na ilitangaza wazi kugoma kuondoka huko kaskazini mwa Iraq, hata hivyo baadaye ilitoa ahadi ya kuondoa askari wake hao.
Hata hivyo kama alivyosema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Ibrahim al-Jaafari, licha ya Uturuki kuahidi suala hilo, bado hadi sasa askari hao hawajaondoka eneo la kaskazini mwa nchi hiyo. Inaonekana kwamba serikali ya Uturuki haina nia ya kuondoa askari wake kutoka kambi ya kijeshi ya Bashiqa. Hii ni kwa kuwa lengo la Ankara katika hatua yake hiyo ni kupenyeza satwa yake ya kijeshi nchini Iraq na Syria na inatumia hali ya machafuko ya hivi sasa kufikia malengo yake hayo. Kwa mujibu wa weledi wa mambo madhumuni ya kutumwa askari wa Uturuki kaskazini mwa Iraq, ni kujaribu kuanzisha kambi mpya ya kijeshi katika nchi nyingine ili kwa njia hiyo iweze kuimarisha ushawishi wake wa kijeshi. Katika hali ambayo viongozi wa Uturuki hivi sasa wanafuata mienendo hiyo ya kichokozi, awali viongozi hao kwa kupitia siasa za kuboresha uhusiano mwema na majirani zake, ilipelekea taifa hilo kustawisha mahusiano na nchi jirani.
Hata hivyo siasa za hivi karibuni za Ankara kuhusu Iraq na Syria, zimeibua migogoro katika mahusiano na majirani wake na hata katika eneo zima la Mashariki ya Kati. Ushahidi unaonyesha kuwa, misimamo ya Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki imechangia kuchochea migogoro katika siasa za kigeni za serikali ya Ankara kiasi cha askari wa nchi hiyo kufikia kutungua ndege ya kijeshi ya Russia aina ya Sukhoi Su-24. Hata hivyo baada ya kutokea jaribio la mapinduzi ya kijeshi mwezi Julai mwaka jana, serikali ya Ankara iliiomba radhi Russia kwa kitendo chake hicho.