UN: Yemen imerejea muongo mmoja nyuma katika sekta ya afya
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i24535-un_yemen_imerejea_muongo_mmoja_nyuma_katika_sekta_ya_afya
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umesema sekta ya afya ya Yemen imesambaratika kwa kiwango cha kutia wasi wasi kutokana na hujuma za kila siku za jeshi la utawala wa Aal-Saud.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 01, 2017 00:52 UTC
  • UN: Yemen imerejea muongo mmoja nyuma katika sekta ya afya

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umesema sekta ya afya ya Yemen imesambaratika kwa kiwango cha kutia wasi wasi kutokana na hujuma za kila siku za jeshi la utawala wa Aal-Saud.

Meritxell Relano, mwakilishi wa UNICEF nchini Yemen amesema kuwa, mashambulizi na mgogoro wa kiuchumi nchini Yemen umeisababisha nchi hiyo irejee nyuma katika sekta ya afya, zaidi ya ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.

Afisa huyo wa UN amesema kuwa, kati ya watoto 1000 wanaozaliwa katika nchi hiyo masikini ya Kiarabu, 63 hupoteza maisha kabla ya kufikisha miaka mitano, kutokana na kusambaratika kikamilifu mahospitali, zahanati na suhula za matibabu.

Hospitali ya Abs nchini Yemen baada ya kushambuliwa na Saudia 

Amesema mafanikio katika uga wa afya yaliyokuwa yamepigwa na nchi hiyo ndani ya muongo mmoja yamevurugika kutokana na mgogoro na mashambulizi yanayoikabili nchi hiyo ya Peninsula ya Kiarabu.

Itakumbukwa kuwa mwezi Machi mwaka 2015, Saudi Arabia ikiungwa mkono na Marekani ilianzisha mashambulio dhidi ya maeneo mbalimbali ya Yemen. Moja kati ya malengo makuu ya mashambulio hayo ya kivamizi ya utawala wa Aal Saud ni kutaka kumrejesha madarakani kibaraka wake, rais aliyejiuzulu na kuitoroka nchi Abdrabbuh Mansur Hadi.

Uvamizi na mashambulizi ya jeshi la Saudi Arabia na waitifaki wake yaliyoanza yapata miaka miwili na nusu iliyopita yameua zaidi ya watu 11,000 wa Yemen wengi wao wakiwa wanawake na watoto wadogo, mbali na kuvuruga asilimia kubwa ya miundomsingi.