Rais Aoun: Hizbullah inailinda Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i25046-rais_aoun_hizbullah_inailinda_lebanon
Rais Michel Aaoun wa Lebanon amesisitiza kuwa silaha za Hizbullah hazina mgongano na uhalali wa serikali bali silaha hizo ni sehemu kuu na ya msingi ya ulinzi wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 12, 2017 12:33 UTC
  • Rais Aoun: Hizbullah inailinda Lebanon

Rais Michel Aaoun wa Lebanon amesisitiza kuwa silaha za Hizbullah hazina mgongano na uhalali wa serikali bali silaha hizo ni sehemu kuu na ya msingi ya ulinzi wa nchi hiyo.

Rais wa Lebanon ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya CBC ya Misri kabla ya safari yake anayotazamiwa kuifanya nchini humo na kubainisha kuwa sehemu ya ardhi ya Lebanon imevamiwa na kukaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel; na jeshi la Lebanon halina uwezo wa kutosha wa kupigana vita na utawala huo; kwa sababu hiyo serikali inahisi ulazima wa kuwepo silaha za muqawama kwa ajili ya kukamilisha uwezo wa kisilaha wa jeshi.

Wanamuqawama wa Hizbullah

Aoun ameongeza kuwa Hizbullah ni chemchemi ya utulivu kwa serikali na wananchi wa Lebanon.

Katika mahojiano hayo, Rais wa Lebanon ametilia mkazo kutatuliwa kisiasa mgogoro wa Syria na kueleza kwamba kushindwa kutatuliwa mgogoro huo kwa njia za amani kumeiteketeza nchi hiyo.

Katika mahojiano mengine aliyofanyiwa na gazeti la Misri la al-Ahram ambayo yamechapishwa katika toleo la leo la gazeti hilo, Rais wa Lebanon amelaani jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na kusisitiza kuwa endapo utawala wa Kizayuni utafuta utambulisho wa Palestina itakuwa aibu ya kihistoria kwa Waarabu.

Aoun ameeleza pia kwamba nchi za Magharibi zimeanzisha mgogoro katika eneo la Mashariki kwa ajili ya kufikia malengo na maslahi yao na kuongeza kuwa nchi za Kiarabu zinaweza kufikia suluhu kwa njia ya maelewano au kwa uchache kutekeleza usitishaji vita na kurejesha utulivu baina yao.

Rais wa Lebanon kesho Jumatatu anatazamiwa kufanya safari nchini Misri na siku ya Jumanne ataelekea Jordan kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hizo…/