Feb 26, 2017 08:06 UTC
  • Maulamaa wa Bahrain wasisitiza kumuunga mkono Sheikh Issa Qassim

Maulamaa nchini Bahrain wametoa taarifa na kusisitiza udharura wa kumtetea na kumuunga mkono Ayatullah Sheikh Issa Qassim, mwanazuoni maarufu wa Kiislamu nchini humo anayekandamizwa na utawala wa ukoo wa Aal Khalifa.

Katika taarifa, wanazuoni hao wa Bahrain wameuonya vikali utawala wa Aal Khalifa kutothubutu kuchukua hatua yoyote ya kijinga ya kumhujumu Sheikh Issa Qassim. Aidha wameutaka utawala huo wa kiimla kuacha kuvunjia heshima matukufu ya kidini na kurejea katika mkondo wa akili na mantiki sambamba na kusikiliza matakwa ya wananchi.

Taarifa hiyo imesema:"Wananchi wana azma imara na thabiti na wako tayari kujitoa muhanga kwa ajili ya kumtetea kiongozi wao."

Tamko hilo limetolewa katika hali ambayo kesho, 27 Februari kesi ya Sheikh Issa Qassim itasikilizwa baada ya kuahirishwa mara kadhaa. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Bahrain inadai kuwa Sheikh Issa Qassim anahudumia madola ajinabi na kuibua hitilafu za kimadhehebu na kwa msingi huo Juni 20 mwaka jana ulimpokonya uraia.

Wanazuoni wa Kiislamu nchini Bahrain

Tokea wakati huo,wananchi wa Bahrain wamekuwa wakikusanyika nje ya nyumba ya Sheikh Qassim kumuunga mkono na kumlinda asidhuriwe na askari wa ufalme ambao wameizingira nyumba yake.

Tangu mwezi Februari mwaka 2011, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya kupinga utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal-Khalifa, kushinikiza uhuru na kutekelezwa uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuweko madarakani utawala uliochaguliwa na wananchi wenyewe. Hata hivyo utawala wa Aal Khalifa umekuwa ukijibu matakwa ya wananchi hao kwa mkono wa chuma na ukandamizaji mkubwa.

Tags