Jibu la Syria kwa uzushi wa magaidi na waungaji mkono wao
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Faisal al-Miqdad ametaka wahusika wa mashambulio ya silaha za kemikali yaliyofanywa katika mkoa wa Idlib wawajibishwe na kusisitiza kuwa jeshi la Syria halijawahi hata mara moja kutumia silaha za kemikali katika vita na magaidi.
Faisal al-Miqdad ametangaza kuwa Syria imetekeleza ahadi zake katika kutoa ushirikiano kwa Shirika la Kuzuia Uenezaji Silaha za Kemikali; na ushirikiano huo iliotoa umethibitishwa na shirika hilo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amesema, ushindi uliopatikana Halab (Aleppo) na mafanikio liliyopata jeshi la Syria kandokando mwa mji mkuu Damascus na katika mji wa Hama ndio sababu iliyowafanya magaidi na waungaji mkono wao washambulie mkoa wa Idlib ulioko kaskazini magharibi mwa nchi hiyo kwa silaha za kemikali.
Faisal al-Miqdad amesisitiza kuwa jamii ya kimataifa inapaswa iwawajibishe wale waliohusika na jinai ya shambulio la silaha za kemikali mjini Idlib.
Huku akiashiria kwamba mnamo wiki kadhaa zilizopita kundi la kigaidi la Jabhatu-Nusra liliingiza nchini Syria shehena ya mada za kemikali, Naibu Waziri wa Mambo ya nje wa nchi hiyo amesema, serikali ilitoa taarifa kwa Shirika la Kuzuia Uenezaji Silaha za Kemikali kuhusu uingizwaji wa shehena hiyo.
Duru za habari zenye mfungamano na magaidi na wapinzani wa Syria alfajiri ya kuamkia juzi Jumanne zilidai kwamba, ndege kadhaa za kijeshi zimefanya hujuma ya kuushambulia mji wa Khan Sheikhoun ulioko mkoani Idlib kwa makombora yenye gesi ya sumu inayofanya kazi sawa na gesi ya sumu ya sarin.
Makao makuu ya jeshi la Syria pia yamekanusha kutumiwa na jeshi hilo mada na silaha za kemikali na kutangaza kuwa makundi ya kigaidi ndiyo yanayobeba dhima ya shambulio hilo la kemikali.
Lengo la kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh la kutumia kwa wingi siaha za kemikali ni kuzuia lisishindwe kikamilifu na kuzusha woga na hofu kwa wananchi ili wasalimu amri kwa matakwa na tamaa zao. Katika mazingira kama hayo nchi zinazounga mkono magaidi kama Uturuki, Saudi Arabia na Qatar pamoja na baadhi ya madola ya Magharibi haziko tayari kusimamisha mashambulio ya kila upande ya magaidi hao; na kivitendo zinawepesisha njia za kuwawezesha kuzipata silaha za kemikali.
Nukta ya kutaamali hapa ni kwamba, kwa msaada wa nchi za Magharibi na waitifaki wao wa Kiarabu, magaidi, ambao wametenda jinai dhidi ya binadamu nchini Syria wanajaribu kutafuta njia za kuzihusisha jinai zao hizo na serikali ya Damascus. Kwa kutumia mbinu za hila na hadaa, waungaji mkono wa magaidi nchini Syria wanajaribu kupindua juu chini ukweli halisi wa matukio yanayojiri nchini humo.
Serikali ya Syria inaandamwa na njama za Magharibi kuhusu ukiukaji haki za binadamu katika hali ambayo kulingana na azimio nambari 2118 lililopitishwa mwezi Septemba 2013 na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mada za kemikali za Syria zilishakabidhiwa kwa Shirika la Kuzuia Uenezaji Silaha za Kemikali; na serikali ya nchi hiyo imetoa ushirikiano unaotakiwa katika suala hilo.
Lakini katika upande mwengine kuna ripoti kadhaa zinazoonyesha kuwa nchi za Magharibi zinaendelea kuwapatia silaha za kemikali magaidi, hatua inayotafsiriwa kama utoaji baraka kamili Magharibi kwa magaidi hao ili washadidishe jinai zao wanazofanya nchini Syria.
Matukio yanayojiri Syria yanaonyesha kuwa kutokana na kuzidi kubadilika mlingano wa nguvu katika medani za vita kwa manufaa ya mfumo wa wananchi unaotawala nchini humo na kuzidi kupata ushindi na mafaniko jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi dhidi ya magaidi, duru mpya ya njama na propaganda imeanza dhidi ya nchi hiyo. Kwa tathmini ya duru za habari za Syria, lengo la waungaji mkono wa magaidi la kuzusha madai bandia dhidi ya serikali ya Damascus ni kuandaa mazingira ya kuwawezesha magaidi hao watumie zaidi silaha za kemikali ili kuzuia wasisambaratishwe na kushindwa kikamilifu nchini humo.
Kuhusiana na nukta hiyo kituo cha Marekani cha utafiti kuhusu magaidi wa kundi la ukufurishaji la Daesh (ISIS) kiitwacho IHS kimetangaza kuwa mwaka 2014 magaidi hao walitumia silaha za kemikali zaidi ya mara 71 katika nchi za Iraq na Syria.
Duru za sheria sio tu zimewakosoa wapinzani wabeba silaha nchini Syria lakini zinasisitiza pia kwamba makundi hayo hayajajiwekea mpaka wowote katika jinai na mauaji yanayofanya; na kutokana na uelegevu unaoonyeshwa na jumuiya za kimataifa yanajihisi yako huru kikamilifu kufanya vitendo vya kigaidi na kutenda jinai za kivita na yana usalama kamili wa kutofuatiliwa kwa namna yoyote ile kisheria.../